1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Afrika Kusini kupoteza mshahara, kutumia ndege vibaya

28 Septemba 2020

Waziri wa ulinzi wa Afrika Kusini amekosolewa vikali  na atapoteza mshahara wake kwa miezi mitatu baada ya maafisa wa chama tawala nchini humo kusafiri kwa ndege ya jeshi la wanaanga kwenda Zimbabwe mwezi huu.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa in Pretoria
Picha: AFP/P. Magakoe

Hatua hiyo imeelezwa na Rais Cyril Ramaphosa siku ya Jumapili. Hatua ya ujumbe wa chama cha African National Congress ANC kusafiri kwa  ndege hiyo ya jeshi kumezusha ukosoaji mkubwa kuhusiana na matumizi ya mali ya serikali kwa shughuli za chama.

Ziara hiyo ya ujumbe wa ANC nchini Zimbabwe ilikuwa ya kushiriki mazungumzo na Chama tawala cha Zimbabwe,Zanu Pf ambayo yalilenga kukisaidia chama hicho kuyatatua matatizo ya kisiasa ya nchi yake pamoja na matatizo ya kiuchumi.

Wajumbe hao walipanda ndege ya waziri wa ulinzi Nosiviwe Mapisa Nqakula badala ya kusafiri kibinafsi.Waziri huyo alikuwa amepanga kuwa na mkutano nchini Zimbabwe kujadili masuala ya kikanda kufuatia mkutano wa hivi karibuni wa kilele wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC.

Rais Ramaphosa amesema anataraji chama cha ANC kitaifidia serikali kutokana na tukio hilo. Chama cha upinzani nchini humo cha Democratic Alliance DA kimemtaka waziri huyo ajiuzulu.