1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wa Israel lazima uhakikishwe

20 Julai 2015

Makamu wa Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameeleza wazi kwamba kutambuliwa kwa haki ya Israel ya kuendelea kuwa salama ndiyo msingi wa kujenga uhusiano endelevu baina ya Ujerumani na Iran.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel alakiwa na wenyeji wake nchini Iran
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel alakiwa na wenyeji wake nchini IranPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Gabriel amesema ni wazi kwamba yeyote anaetaka uhusiano endelelevu na Ujerumani hana budi aitambue haki hiyo ya Israel

Katika siku ya pili ya ziara yake ya kihistoria nchini Iran Bwana Gabriel ambae pia ni Waziri wa uchumi na nishati leo anakutana na Rais wa nchi hiyo Hassan Rouhani ,mawaziri, Gavana wa Benki Kuu na wawakilishi wa Baraza la viwanda na biashara la Iran.

Bwana Gabriel ni kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu kutoka nchi za magharibi kwenda Iran tangu nchi hiyo ifikie mapatano na mataifa makubwa duniani juu ya mpango wake wa kinyuklia.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa Iran itasimamisha kwa muda wa miaka 10 shughuli za kurutubisha madini ya Uran, na kwa hatua hiyo, jumuiya ya kimataifa itaviondoa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Iran, hatua kwa hatua.

Makamu huyo wa Kansela ameiita ziara yake nchini Iran kuwa ni hatua muhimu.

Jadi ya uhusiano mzuri:
Amesema pana jadi ya uhusiano mzuri baina ya Ujerumani na Iran na wajasiriamali wengi wa Ujerumani wanataka kuyaunganisha tena mawasiliano ya hapo zamani.

Bwana Gabriel ameeleza kuwa hali hiyo itawezekana ikiwa yale yaliyofikiwa na Iran yatatekelezwa kuanzia mwaka ujao.

Hata hivyo bwana Gabriel amesema bado pana hatua nyingine nyingi zinazopaswa kuchukuliwa.

Kwa mara ya mwisho ujumbe wa Ujerumani ulioongozwa na Waziri wa fedha wa hapo awali Hans Eichel ulikuwapo nchini Iran miaka 13 iliyopita.

Katika ziara yake Waziri Gabriel anaongozana na wawakilishi wa sekta ya uchumi.

Baraza la viwanda na biashara la Ujerumani limebashiri kwamba Ujerumani itaweza kuiuzia Iran bidhaa zenye thamani ya Euro Bilioni tano mnamo kipindi cha miaka miwili tu na kuongezeka hadi kufikia Euro Bilioni 10.

Leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litajadili suala kuondolea Iran vikwazo. Baraza hilo linatarajiwa kukubaliana juu ya hatua hizo.

Lakini haina maana kwamba hatua zote zilizochukuliwa ili kuiadhibu Iran zitaondolewa mara moja .

Shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia duniani IAEA pia linapaswa kuhakikisha kwamba Iran kwa upande wake inayatekeleza yaliyofikiwa.

Kwa kufanya ziara hiyo nchini Iran ambako amefuatana na ujumbe mkubwa wa wawakilishi kutoka sekta za uchumi na biashara, Waziri Gabriel anatoa ishara thabiti kwamba Ujerumani inadhamiria kuujenga upya uhusiano wake wa kisiasa na kiuchumi na Iran.

Mwandishi:

Mwandishi: Mtullya abdu/rtre/ dpa,

Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW