Waziri Kiongozi wa Scotland atangaza kujiuzulu
29 Aprili 2024Hatua iliyochukuliwa na Humza Yousaf inaashiria anguko la kushangaza la chama tawala Scotland cha SNP na inaimarisha nafasi ya chama cha upinzani cha Labour katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi unaotarajiwa mwaka huu.
Yousaf alisema anajiuzulu baada ya wiki iliyoshuhudia mivutano ya kisiasa iliyosababishwa na serikali yake kufuta makubaliano ya muungano na chama cha kijani.
Aidha alishindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha ili kunusurika katika kura ya kutokuwa na imani naye ambayo ilikuwa inatarajiwa baadaye wiki hii.
Yousaf amesisitiza kwamba ili kuirekebisha migawanyiko ya kisiasa iliyojitokeza ni muhimu akiwepo mtu mwingine kwenye uongozi.
"Kwa bahati mbaya, katika kuhitimisha mkataba wa serikali kwa namna ambayo nilifanya sikuzingatia kiwango cha kuumizwa na kufadhaika nilichowasababishia wenzangu wa Chama cha Kijani. Na ingawa nilikuwa na njia ya kuiepuka hoja ya wiki hii ya kutokuwa na imani nami, siko tayari kubadilishana maadili na kanuni zangu, au kufanya makubaliano na yeyote, kwa ajili ya kubaki na mamlaka," amesema Humza katika ujumbe wake wa kutangaza kujiuzulu.
Nini kimekwenda kombo kwa mwanasiasa wa kwanza muislamu kuiongoza Scotland?
Ni kiongozi wa kwanza wa Kiislamu wa chama kikuu cha kisiasa cha Uingereza, na kiongozi mdogo kabisa wa Scotland aliyewahi kuchaguliwa, ameongoza kwa muda mfupi.
Yousaf, ambaye Chama chake cha Scotland National Party SNP, kimedhoofishwa na kashfa inayohusu ufadhili wakati wa kampeini za uchaguzi pamoja na mgawanyiko juu ya haki za watu waliobadili jinsia, amejiuzulu baada ya kushindwa kufanya makubaliano na chama kilichojitenga na ambacho kiti chake kimoja kingeweza kumpa wingi wa viti kwenye bunge kwenye la Scotland.
Uteuzi wake ulifuatia kupanda kwake kwa kasi katika chama cha SNP tangu alipokuwa mbunge kwa mara ya kwanza na kuhudumu serikalini tangu 2012 katika majukumu yakiwemo waziri wa uchukuzi na waziri wa masuala ya sheria.
Mwaka mmoja baada ya kushinda kiti, alifanywa waziri wa Ulaya na maendeleo ya kimataifa.
Aliyekuwa waziri kiongozi Nicola Sturgeon alipotangaza kujiuzulu mnamo 2023, Yousaf alionekana kama mtu anayeweza kumrithi.
Mwaka mmoja baadaye alichukua nafasi ya Nicola Sturgeon kama waziri kiongozi na mwenyekiti wa chama cha SNP.
Amekuwa waziri kiongozi wa kwanza mwenye umri mdogo tangu kuundwa kwa bunge la Scotland baada ya mageuzi ya kimajimbo mwaka 1999 na kiongozi wa kwanza wa Kiislamu wa chama hicho kikubwa kabisa nchini Uingereza.
Alipochukua wadhifa huo kuliibuka mjadala kuhusiana na iwapo ushindi wake unaashiria enzi ama kawaida mpya nchini Uingereza na hasa kwa kuzingatia kwamba taifa hilo kwa sasa linaongozwa na waziri mkuu Rishi Sunak, mwenye asili ya India.
Amesema ataendelea kushikilia nafasi hiyo hadi atakapochaguliwa mrithi baada ya uchaguzi wa uongozi wa SNP.