Waziri mkongwe wa Tanzania William Lukuvi afariki dunia
25 Machi 2026
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samiam Suluhu Hassan, wadau wa siasa, wabunge na viongozi katika kada mbalimbali hapa nchini, wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mbunge wa Isimani na Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu, Bunge na Walemavu, William Lukuvi.
Lukuvi amefariki dunia kwa mshtuko wa moyo. Lukuvi atakumbukwa kama miongoni mwa viongozi waliohudumu bungeni kwa miongo zaidi ya mitatu.
Taifa la Tanzania limeamshwa na msiba mzito wa Mbunge wa Isimani, William Vangimembe Lukuvi, anayetajwa kama miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa serikalini na waliohudumu katika bunge tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi Tanzania mwaka 1995.
Salamu za rambirambi za Rais Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan,ametuma salamu zake za rambirambi kupitia ukurasa wake wa X, akimtaja Lukuvi kama kiongozi mwenye uzoefu, mzalendo na mtumishi wa umma aliyelitumikia Taifa kwa uadilifu, weledi na kujitolea.
Viongozi wa CCM, nao wamemzungumzia, Lukuvi kama mwadilifu na mwenye uzoefu. Aliyekuwa mbunge wa Geita Constatine Kanyasu ambaye pia amewahi kufanya kazi kwa ukaribu na Lukuvi ameiambia DW.
Lukuvi ambaye amefariki leo asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, alikuwa Bungeni kwa kipindi cha Saba ikiwa ni tangu Mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi wa Mfumo wa Vyama Vingi nchini.
Zaidi ya miongo mitatu ya utumishi bungeni
Lukuvi, amekuwa mbunge miongo mitatu na Waziri kwa miaka 31, na pia ni miongoni mwa mawaziri walioaminika na awamu tatu za tawala tafauti katika kuongoza wizara kadhaa, ikiwemo ile ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ikielezwa kuwa alikuwa na uzoefu nayo.
Hilo na mengine vilimfanya Lukuvi kuwa miongoni mwa wabunge wakongwe katika bunge la 13, Mbunge wa Kilolo, Rita Kabati, amezungumzia Lukuvi na kusema ni miongoni mwa viongozi waliofia nchi.
Lukuvi anatajwa kama mwanasiasa aliyelelewa na kukulia ndani ya CCM, akianzia Umoja wa Vijana (UVCCM) na kuingia bungeni mwaka 1995. Ameshika nafasi mbalimbali za uwaziri ikiwamo Waziri wa Sera, Uratibu,Bunge mpaka mauti yanamfika.
DW Dar es Salaam