Waziri mku wa Italia ziarani mjini Berlin
30 Aprili 2013Ziara ya kwanza rasmi ya waziri mkuu wa Italia Enrico Letta nchi za nje inafanyika siku moja tu baada ya waziri mkuu huyo mpya kusema serikali yake ya muungano itazipindua haraka hatua za kufunga mkaja.Matamshi hayo ameyatoa katika hotuba yake ya ufunguzi bungeni-hotuba iliyofuatiliziwa kwa makini na washirika wa Italia katika umoja wa ulaya,ikiwa ni pamoja na Ujerumani,inayokamata usukani wa hatua za kupunguza matumizi barani ulaya.
"Italia inaangamia kutokana na hatua za kufunga mkaja.Sera za kuhimiza ukuaji wa kiuchumi haziwezi kusubiri" amesisitiza.
Mwaasiasa huyo anaefuata siasa ya wastani ya mrengo wa shoto,aliyekabidhiwa hatamu za uongozi miezi miwili ya uchaguzi mkuu,ameahidi "kuipatia fanaka nchi hiyo inayokabwa na hali mbaya ya kiuchumi,miezi 18 kutoa sasa la sivyo "atajibebesha dhamana ya kushindwa juhudi zake."
Ulaya,injini endelevu ya ukuaji wa kiuchumi
Mjini Berlin waziri mkuu mpya wa Italia Enrico Letta atalahikiwa kwa heshima za kijeshi kabla ya kukutana na waandishi habari leo jioni na kufuatiwa na mazungumzo na karamu ya chakula cha usiku pamoja na kansela Angela Merkel anaetetea hatua za kufunga mkaja kama njia ya kuondokana na nakisi na kupunguza madeni.
Baadae atakwenda Brussels kuzungumza pamoja na rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy.
Nchini Italia kwenyewe,baraza la Senet limeanza kujadili mpango wa serikali ya waziri mkuu huyo kabla ya kupiga kura ya kuwa na imani au la na serikali yake.
Mpango huo umeshaidhinishwa na bunge kwa kura 453 kwa 153 .Enrico Letta amewaambia wabunge hali ya kiuchumi ya Italy bado si nzuri kukiwa na mzigo wa madeni yapatayo Euro trilioni mbili mabegani mwa wananchi wa kawaida wa nchi hiyo.
Hata hivyo ameimulika pia Ulaya akisema inabidi irejee kuwa injini indelevu ya ukuaji wa kiuchumi-akigusia dhamiri yake ya kuutanabahisha Umoja wa Ulaya uipindue sera yake inayozusha mabishano ya kufunga mkaja.
Mwanasiasa huyo wa chama cha Democratic amesema anataka kulishughulikia haraka suala la mmomonyoko mbaya kabisa wa kijamii kuwahi kushuhudiwa tangu miaka 20 iliyopita huku idadi ya wasiokuwa na kazi ikifikia asili mia 11.6.Amesema pia ataisitisha kodi ya nyumba iliyoanzishwa na waziri mkuu wa zamani Mario Monti kuanzia mwezi June mwaka huu.
Hotuba ya waziri mkuu mpya wa Italia imetuliza hali ya mambo katika masoko ya hisa mjini Milan na pia mjini New York.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel