Waziri mkuu Abe aitembelea Pearl Harbor
27 Desemba 2016Viongozi hao wawili watatembelea kituo cha manowari ya kivita kisiwani humo ambako mwaka 1941 uvamizi wa Japan uliipelekea Marekani katika vita ya pili ya dunia. Abe aliyewasili jana Hawaii, alitembelea makuburi ya kumbukumbu ya kitaifa ya Pasifiki na kuweka shada ya maua. Shinzo Abe amesema "chini ya muungano wa matumaini, ninavyoweza kuuita, ninaamini kwamba Japan na Marekani zitafanya kazi pamoja kuelezea changamoto kadhaa sio tu za kikanda bali pia za kimataifa".
Ziara hiyo ya baada ya miaka 75 tangu Japani ilipofanya mashambulizi ya kushtukiza inalenga kuonyesha mahusiano baina ya nchi hizo mbili na ziara ya rais Obama mwezi Mei katika eneo la Hiroshima ambako Marekani ilidondosha bomu la kwanza la atomiki.
Manowari ya kivita
Viongozi hao watazuru mabaki ya manowari ya kivita ya USS Arizona ambamo mabaharia 1,177 pamoja na wanamaji walikufa. Mabaki ya manowari hiyo bado yanaonekana mpaka leo. Kwa mujibu wa maafisa wa seikali wa Japan, waziri mkuu Abe hatoomba radhi kwa shambulizi la Desemba 7 mwaka 1941. Shambulizi hilo liliwaua wamarekani 2403.
China hata hivyo imeikosoa ziara ya waziri mkuu Abe ikiita ni "ishara ya kujidai", na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Japan, Hua Chunying anasema bila ya kuwepo na maridhiano ya amani na China na wahanga wengine barani Asia, Japan haiwezi kuacha historia hiyo nyuma.
Umuhimu wa maridhiano
Kiongozi huyo wa Japan anayo matumaini makubwa katika ziara hiyo na rais Obama kwasababu anaamini kuna umuhimu wa kufanya maridhiano na kuwaombea wote waliouawa katika vita.
Ingawa ziara hiyo haitakuwa ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Japan, itakuwa ni ziara muhimu, kwasabau waziri mkuu Abe anasimama sambamba na rais wa sasa wa Marekani kuwakumbuka waliouawa katika vita baina ya mataifa hayo mawili.
Mwezi Mei, Obama alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea Hiroshima, ambako vikosi vya nchi hiyo viliangusha bomu la nyuklia mwishoni mwa vita. Obama hakuomba radhi kwa matendo yaliyofanywa na Marekani lakini alizungumzia umuhimu wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia.
Obama na Abe watafanya mkutano wa pamoja kabla ya kuitembelea manowari ya kivita ya USS Arizona pamoja na kuwahutubia hadhara ya wamarekani, wakazi wa hapo na maafisa wa kijeshi wakiwemo wakongwe na manusura wa shambulio hilo.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef