1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu mpya wa Pakistan aapishwa

Charo, Josephat26 Machi 2008

Wanadiplomasia wa Marekani kukutana na viongozi wa Pakistan

Waziri mkuu mpya wa Pakistan Yousaf Raza GilaniPicha: AP

Waziri mkuu mpya wa Pakistan ameapishwa leo, siku moja baada ya bunge kumchagua. wanadiplomasia wawili wa Marekani wamewasili mjini Islamabad hii leo kwa mazungumzo na rais Pervez Musharraf na waziri mkuu mpya, Yousaf Raza Gilani.

Rais wa Pakistan, Pervez Musharraf, hii leo amemuapisha Yousaf Raza Gilani kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. Gilani, kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha marehemu Benazir Bhutto, alichaguliwa kuwa waziri mkuu hapo jana. Kiongozi huyo alitumikia kifungo cha miaka mitano gerezeni wakati wa utawala wa kijeshi wa Pervez Musharraf lakini leo amejikuta akiapishwa na rais Musharraf kuwa waziri mkuu.

Gilani ameapa ataheshimu uhuru wa Pakistan na kuyalinda maadili ya kiislamu.

´Na kila wakati kwa masilahi ya uhuru, heshima, umoja, uthabiti na maendeleo ya Pakistan, nitajitahidi kuhiyafadhi maadili ya kiislamu ambayo ni msingi wa kuundwa kwa taifa la Pakistan.´

Kelele zilizosema Bhutto aishi milele zimesikika kwa mda mfupi miongoni mwa watu waliohudhuria sherehe ya kuwapishwa Gilani mara tu waziri mkuu huyo, aliyekuwa amevalia vazi la kitamaduni la sherwani, alipomaliza kula kiapo.

Rais Musharraf na waziri mkuu Gilani hawakutoa hotuba baada ya sherehe hiyo iliyodumu muda wa dakika tano katika ikulu ya rais mjini Islamabad.

Wanadiplomasia wa Marekani

Sherehe hiyo imefanyika wakati naibu waziri wa mambo ya ndani wa Marekani, John Negroponte na naibu waziri wa mashauri ya kigeni, Richard Boucher, walipowasili nchini Pakistan kwa mazungumzo na rais Musharraf, waziri mkuu Gilani na waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Nawaz Sharif.

Msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Islamabad, Kay Mayfield, amethibitisha kuwasili kwa viongozi hao wawili wa Marekani na kusema ziara yao ni sehemu ya mfululizo wa ziara ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa Marekani nchini Pakistan. Mayfiled amesema watakutana na viongozi mbalimbali wa Pakistan lakini hakutoa maelezo zaidi.

Naibu waziri wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani John NegropontePicha: AP

John Negroponte na Richard Bouzcher wamekutana na Nawaz Sharif, ambaye aling´olewa madarakani na rais Musharraf mnamo mwaka wa 1999 na ambaae pia ni kiongozi wa chama kidogo katika serikali ya mseto inayoongozwa na chama cha marehemu Benazir Bhutto, cha Pakistan People´s Party, PPP.

Ziara ya viongozi hao wa Marekani nchini Pakistan inafanyika wakati wadhifa wa rais Musharraf ukikabiliwa na mtihani mkubwa tangu aliponyakua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka wa 1999.

Waziri mkuu Gilani pia ameahidi kuilinda na kuitetea katiba ya Pakistan.

´Sitaruhusu masilahi yangu ya kibinafsi kuathiri mwenendo wangu au maamuzi yangu ya kikazi. Nitaihifadhi, kuilinda na kuitetea katiba ya jamhuri ya kiislamu ya Pakistan.´´Katika hali zote nitatenda haki kwa watu wa matabaka yote kwa mujibu wa sheria bila uonga, upendeleo au nia mbaya.´

Waziri mkuu Gilani alitoa changamoto kubwa kwa rais Musharraf dakika chache baadaya kuchaguliwa na bunge hapo jana kwa kuamuru majaji wote waliokamatwa kufuatia amri ya rais wakati alipotangaza utawala wa hatari mnamo mwezi Novemba mwaka jana, waachiwe.

Rais Musharraf, aliyejiuzulu kama kamanda mkuu wa jeshi la Pakistan hapo mwaka jana, alimfuta kazi jaji mkuu pamoja na majaji wengine wapatao 60 kwa hofu kwamba walikuwa na njama ya kubatilisha ushindi wake katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana.

Serikali mpya imeahidi kuwarudisha majaji wote kazini, ambao baadaye wataweza kubatilisha ushindi wa rais Musharraf katika uchaguzi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW