Mrengo wa kushoto waongoza sereikali
26 Januari 2015Serikali mpya ya Ugiriki itaundwa na vyama vinavyopinga hatua za kufunga mkaja kati ya kile cha mrengo wa kushoto cha Syriza kilichojipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa jana jumapili na kile cha wagiriki huru wanaofuata siasa za mrengo wa kulia.Washirika wa Ugiriki wanaisihi itekeleze majukumu yake.
Umoja wa Ulaya umeshaitahadharisha serikali mpya ya Ugiriki inayoongozwa na Alexis Tsipras mwenye umri wa miaka 40,hawako tayari kuifutia madeni nchi hiyo ambayo chama cha Syriza kingependa yajadiliwe upya.
Yadhihirika kana kwamba msimamo mkali mbele ya wafadhili;Umoja wa ulaya na shirika la fedha la kimataifa ndio uliopata ushindi baada ya kutangazwa makubaliano ya kuunda serikali kati ya Syriza na chama kidogo cha wazalendo wa kigiriki wanaojitegemea.
Vyama hivyo viwili kwa pamoja vimejipatia wingi wa viti 162 toka jumla ya viti 300 vya bunge."Kuanzia dakika hii yamechomoza matumaini lakini kwa uangalifu na uadilifu bila ya shangwe" amesema katibu mkuu Podemos Pablo Iglesias baada ya ushindi wa mshirika wake Alexis Tsipras.Pablo Iglesias,mwalimu wa sayansi ya siasa,mwenye umri wa miaka 36 anataraji pia kuibuka na ushindi uchaguzi wa bunge utakapoitishwa nchini Uhispania mwezi Novemba mwaka huu.."Tunaelekea katika hali ambayo inaweza kumwacha peke yake kansela wa Ujerumani Angela Merkel,amesisitiza Iglesias.
Ujerumanai inaweza kufikiria uwezekano wa kushirikiana na serikali mpya ya Ugiriki
Kwa upande wake kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameionya serikali mpya ya Ugiriki inabidi iheshimu majukumu yake kwa wafadhili.
Ujerumani mfadhili mkubwa wa Ugiriki ndani ya Umoja wa Ulaya inasema inaweza kupendekeza kushirikiana na serikali mpya ya Ugiriki huku ikiwa inatafakari mustakbal wake na namna ya kutekeleza ahadi zake."Msemaji wa kansela Angela Merkel Steffen Seibert amewaambia maripota mjini Berlin."Kwa maoni yetu tunaona ni muhimu kwa serikali mpya kuchukua hatua zitakazoiwezesha Ugiriki kuimarisha shughuli zake za kiuchumi" amesema.
Kwengineko barani Ulaya kuna wengi wanaohisi sawa na Pablo Iglesias kwamba ushindi wa Syriza unaashiria mwisho wa siasa ya kufunga mkaja,lakini ni wachache wanaotaka madeni yajadiliwe upya au kwamba Ugiriki ijitoe katika kanda ya Euro.
Mjadala utapamba moto bila ya shaka katika chaguzi kadhaa zitakazofanyika mwaka huu katika nchi kadhaa za Umoja wa ulaya.
Uhispania inajikuta katika hali sawa na hii ya Ugiriki
Waziri mkuu wa Hispania,mhafidhina Mariano Rajoy amempongeza waziri mkuu mpya wa Ugiriki Tsipras na kusema "anataraji matokeo ya uchaguzi yatapelekea kuundwa serikali tulivu itakayoheshimu mwongozo wa Ulaya."
Uhispania pia imelazimika kutangaza hatua za kufunga mkaja na Rajoy pia anakabiliwa na kishindo cha wafuasi wa mrengo wa kushoto uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwezi Novemba mwaka huu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga