Waziri mkuu Sharif ashinikizwa kuondoka madarakani
13 Agosti 2014Maandamano hayo yameandaliwa na mchezaji wa zamani wa mchezo wa kriketi Imran Khan ,pamoja na kiongozi wa kidini Tahir ul Qadri .Waangalizi wa masuala ya kisiasa wanayaangalia maandamano hayo kama jaribio kwa taifa hilo ambalo limeshazoea hali ya kukabiliwa na mapinduzi ya kijeshi.
Mpinzani mkuu wa Nawaz Sharif,Imran Khana anamtaka waziri mkuu huyo aondoke madarakani akidai kwamba uchaguzi wa mei 2013 ulikumbwa na dosari na kwahivyo pana haja kubwa ya kufanyika mageuzi katika mfumo mzimwa wa uchaguzi ambao anasema hauendani na demokrasia.Sharif haungwi mkono na jeshi la Pakistan na kutofautiana kwake na jeshi la nchi hiyo kunatokana zaidi na suala la sera kuhusu suala la Afghanistan pamoja na jinsi suala la aliyekuwa rais wa taifa hilo Pervez Musharaf linavyoshughulikiwa.
Aidha wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kwa upande mwingine wanaliokosa jeshi la taifa hilo hasa kutokana na dhima yao katika vurugu zilizowahi kutokea huko nyuma kwenye majimbo kadhaa.Katika hotuba yake aliyoitowa kupitia televisheni Jumanne waziri mkuu Sharif alisema yuko tayari kutoa nafasi ya kuchunguzwa madai ya udanganyifu wa kura lakini pendekezo lake hilo limekataliwa.
Serikali kwahivyo imeongeza usalama pamoja na kuzifunga barabara mjini Islamabad kuwazuia waandamanaji kuingia katika mji huo hali ambayo imeongeza wasiwasi wa kutokea vurugu.Itakumbukwa kwamba wafuasi kadhaa wa bwana Qadri pamoja na polisi watatu waliuwawa katika maandamano ya hapo kabla. Wengi wa wadadisi wa mambo wanaamini kwamba hatua zitakazochukuliwa na jeshi kuelekea maandamano ya leo ndiyo itakayoamua hatma ya waziri mkuu.Katika mahojiano yake na DW Qadri ameshasema kwamba binafsi haungi mkono hatua ya jeshi kuchukua madarka kwa nguvu.
Ikumbukwe pia kwamba Qadri ambaye ni miongoni mwa watu wenye sauti katika mtandao wa shule za kidini katika nchi nzima ya Pakistan aliwahi kupambana kwa nguvu za umma bila ya mafanikio kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wakati huo Asif Ali Zardari.
Lakini kutokana na uungwaji mkono mkubwa wa maandamano hayo pamoja na kuweko wanasiasa kama Imran Khan katika kampeini hiyo kuna uwezekano mkubwa wa vuguvugu hilo kufanikiwa,wanahisi wanadisi wengi wa masuala ya kisiasa.Wapakistan wameshawishika kumshinikiza bwana Sharif kuondoka madarakani hasa kutokana na kushindwa kwake kukulitatua suala la ukosefu wa umeme wa mara kwa mara,ukosefu wa haki,pamoja na kuporomoka kwa uchumi.
Mwandishi/Shamil Shams/Saumu Yusuf
Mhariri/Josephat Charo