1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Waziri Mkuu wa Ufaransa ajiuzulu chini ya mwezi mmoja

6 Oktoba 2025

Katika kile kinachoonekana kama kimbunga kipya cha kisiasa nchini Ufaransa, Waziri Mkuu mpya Sébastien Lecornu amejiuzulu siku chache tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo, na chini ya mwezi mmoja tangu kuingia madarakani.

Ufaransa Paris 2025 | Sébastien Lecornu katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika kwenye Hoteli ya Matignon
Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa aliyeteuliwa hivi karibuni na Waziri wa zamani wa Ulinzi Sebastien Lecornu akizungumza mwishoni mwa hafla ya makabidhiano kwenye Hoteli ya Matignon mjini Paris mnamo Septemba 10, 2025.Picha: Ludovic Marin/AFP

Ikulu ya Élysée imethibitisha Jumatatu kwamba Rais Emmanuel Macron amekubali ombi la kujiuzulu kwa Lecornu ambaye alikuwa amechukua nafasi ya mtangulizi wake François Bayrou. Hatua hiyo inamfanya Macron kuwa na mawaziri wakuu wanne ndani ya mwaka mmoja pekee – hali inayodhihirisha ukosefu wa utulivu wa kisiasa katika serikali yake.

Mara baada ya tangazo hilo, vyama vya upinzani vilianza mashambulizi makali. Chama cha National Rally kinachoongozwa na mrengo wa kulia kimeitaka serikali kuitisha uchaguzi mpya wa mapema, huku chama cha mrengo wa kushoto France Unbowed kikimtaka Macron naye ajiuzulu kabisa.

Wakosoaji wanasema kujiuzulu kwa Lecornu ni dalili ya kushindwa kwa sera za Macron na kulegalega kwa uongozi wake, hasa baada ya uchaguzi wa mwaka jana uliotoa bunge lililogawanyika vibaya.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia) akizungumza na Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Ufaransa Sebastien Lecornu (kushoto) baada ya kushiriki hafla ya kuweka shada la maua kwenye mnara wa mashujaa wa kitaifa na wafia imani huko Hanoi mnamo Mei 26, 2025.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Habari za kujiuzulu kwa Waziri Mkuu huyo zilitetemesha masoko ya fedha nchini humo. Kielezo cha CAC-40 kilichojumuisha kampuni 40 kubwa za Ufaransa kilishuka kwa karibu asilimia 2 ikilinganishwa na kiwango cha Ijumaa, hatua iliyodhihirisha hofu ya wawekezaji kuhusu mustakabali wa kisiasa na kiuchumi wa taifa hilo.

Mawaziri walioteuliwa wabaki wasimamizi wa muda

Lecornu alikuwa ametangaza baraza jipya la mawaziri usiku uliotangulia kujiuzulu kwake, hali iliyowaacha mawaziri wake wapya katika mkanganyiko wa ajabu. Wengi wao walikuwa bado hawajaapishwa rasmi, lakini sasa wamebaki kuwa wazee wa kazi wa muda (caretaker ministers) wakisimamia shughuli za kila siku hadi serikali mpya itakapoundwa. Waziri wa mazingira Agnès Pannier-Runacher aliandika kwenye mtandao wa X: "Ninakata tamaa na maigizo haya.”

Uamuzi wa Lecornu kumrejesha Bruno Le Maire aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, kama Waziri wa Ulinzi, umekosolewa vikali. Wapinzani wanasema wakati wa uongozi wake wa zamani, nakisi ya bajeti ya taifa iliongezeka kwa kasi jambo linaloibua mashaka juu ya ufanisi wake.

Nafasi nyingine muhimu zilibaki kama zilivyokuwa: Bruno Retailleau aliendelea kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Jean-Noël Barrot alibaki Wizara ya Mambo ya Nje, Gérald Darmanin aliendelea na Wizara ya Sheria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul katika picha na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot, wakati Wadephul alipozuru Paris 18.07.2025.Picha: Thomas Koehler/AA/IMAGO

Tangu uchaguzi wa mapema ulioitishwa na Macron mwaka jana, siasa za Ufaransa zimekuwa na migawanyiko mikubwa. Bunge la Taifa lina wabunge zaidi ya 320 kutoka vyama vya mrengo wa kulia na kushoto, huku kambi ya Macron na washirika wake wa kihafidhina ikiwa na viti 210 pekee.

Mustakabali wa Macron watiwa shaka

Kabla ya kujiuzulu, Lecornu alijaribu kupunguza joto la kisiasa kwa kufanya mashauriano na vyama vyote vya siasa na vyama vya wafanyakazi. Aliahidi kutozitumia nguvu maalum za kikatiba ambazo watangulizi wake walitumia kupitisha bajeti bila kura ya bunge, akisisitiza kuwa angechagua njia ya maelewano kati ya wabunge wa pande zote.

Kujiuzulu kwa Lecornu kunamwacha Rais Emmanuel Macron katika hali ngumu kisiasa, huku wito wa uchaguzi mpya au kujiuzulu kwake ukiongezeka. Wengi nchini Ufaransa sasa wanahoji kama rais huyo anaweza bado kudhibiti uongozi katika taifa lililogawanyika, linalokumbwa na mivutano ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW