1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu Uingereza Boris Johnson akimbiwa na kakaake

5 Septemba 2019

Kakaake Boris Johnson, Jo Johnson amejiuzulu kwenye serikali kama waziri wa elimu na pia mbunge kufuatia mvutano wa kisiasa ulioitinga nchi hiyo kuhusiana na kujitowa katika Umoja wa Ulaya

Boris Johnson und Jo Johnson
Picha: picture-alliance/ZumaPress/A. Parsons

Uingereza iko katika hali ya mkanganyiko wa kisiasa kuhusu suala la Brexit. Waziri mkuu Boris Johnson anatapatapa  kutafuta njia mpya za kuitisha uchaguzi wa mapema baada ya kushindwa bungeni jana. Leo hii amepata pigo jingine tena.Waziri wake wa sayansi na elimu ambaye ni nduguye amejiuzulu kwenye serikali yake.

Waingereza wamegawika kuhusu suala la kujiondowa Umoja wa Ulaya na suala hilo limemgharimu waziri mkuu Boris Johnson kukimbiwa mpaka  na kakaake mwenyewe. Jo Johnson ametangaza leo kwamba anajiondowa katika nafasi yake ya waziri wa elimu na ubunge pia anajiuzulu. Anasema amechukua uamuzi huo kwasababu amejikuta kwenye njia panda kati ya kuwa mtiifu kwa familia na maslahi ya taifa.

Bunge la UingerezaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Dunham

Katika ujumbe wake wa twita ameandika kwamba  ''ni mvutano usiotatulika na ni muda wa watu  wengine kutwaa majukumu yangu kama mbunge na waziri''. Jo Jonson yeye alipinga kuondoka Umoja wa Ulaya wakati wa kampeini ya kura ya maoni kuhusu Brexit mwaka 2016 na baadae aliwahi kusema Uingereza haipaswi kuondoka kwenye jumuiya hiyo bila ya makubaliano.

Lakini Julai alikubali kuingia kwenye serikali iliyoundwa na kakake anayepigania Uingereza ijitoe Umoja wa Ulaya Oktoba 31 kwa namna yoyote ile. Boris Johnson yuko mbioni hivi sasa, anapanga kuanzisha kile kinachoonekana kuwa ni kampeini ya uchaguzi huku akisema bunge ni adui wa Brexit.John McDonnell waziri kivuli wa fedha kutoka chama cha Labour anasema

''Kwa hakika mawazo yangu kwa Boris Johnson ni kwamba anatakiwa kuwa kama waziri mkuu wa Uingereza.Sisi hatutaki kuwa na mtu anayeonekana kama Donald Trump namba mbili katika nchi hii. Kwa nia njema anatakiwa abadili lugha yake. Hii ni tabia ya kitoto kwa upande wake''

Picha: picture-alliance/dpa/AP/House of Commons/J. Taylor

Serikali ya Uingereza inasema itajaribu tena wiki ijayo kupata njia za kuitisha uchaguzi. Kiongozi wa shughuli za bunge kutoka chama cha Conservative Jacob Rees Mogg anasema kura itapigwa jumatatu juu ya muswada unaotaka uchaguzi wa mapema. Kumekuwa na atiati zinazoenea miongoni mwa waandishi habari huenda waziri mkuu Johnson akajiuzulu ili kuchochea uchaguzi mkuu wa mapema.Lakini mmoja wa mawaziri wake Michael Gove amezipuuza tetesi hizo akisema hafikirii waziri mkuu ana dhamira hiyo ya kujiuzulu.

Umoja wa Ulaya unawasiwasi na hali ya uhusiano wa baadae na Uingereza. Hata hivyo msemaji wa tume ya Umoja wa Ulaya Mina Andreeva anasema.

''Kama nilivyoeleza mara kadhaa nyuma,hatutotowa maelezo ya mara kwa mara kuhusu mikutano hii tutakayoendelea kuwa nayo katika awamu ya kiufundi.Pande zote zimeamua kukutana ijumaa na mazungumzo yapige hatua tutahitaji kupata mapendekezo thabiti yanayoendana na makubaliano ya kujitowa.''

Mpaka sasa Uingereza haijawasilisha mapendekezo yoyote kuhusu suala la Mpaka wa Ireland.Waziri wa uchumi wa Ujerumani Peter Altmeier amemtolea mwito Boris Johnson awasilishe mapendekezo juu ya uhusiano utakaokuwepo na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit akisema pande zote zitakabiliwa na mzigo.

Boris Johnson anasubiriwa kutowa hotuba yake akiwa Kaskazini mwa England,ambayo inaangaliwa kama hotuba ya kampeini ya uchaguzi anaoulazimisha akitarajiwa kuwashambulia wanasiasa na kushinikiza warudi kwa wananchi kuwapa nafasi ya kuamua wanachokitaka.

Mwandishi-Saumu Mwasimba

Mhariri:Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW