Waziri mkuu wa Bosnia-Herzegovina ajiuzulu
1 Novemba 2007Bwana Spiric alisema amekabidhi barua yake ya kujiuzulu kwa rais wa Bosnia.
Nikola Spiric alisema alilazimishwa kuchukuwa hatua hiyo kwa sababu ya mabadiliko yalioanzishwa mwezi uliopita na Miroslav Lajcak, mwakilishi mkuu wa jamii ya kimataifa katika Bosnia. Hatua za mwakilihi huyo, ambazo zinalenga kuboresha uchapaji kazi katika serekali kuu ya Bosnia, zimesababisha hasira miongoni mwa viongozi wa Bosnia ambao wamesema zitapunguza ushawishi wao katika ngazi ya serekali ya shirikisho na kuruhusu Waislamu kudhibiti madaraka.
Mzozo huu wa kisiasa ni mbaya kabisa katika Bosnia tangu kumalizika vita vya kikabila vya mwaka 1992 hadi 1995, na ambavyo vilimalizwa kwa kupatikana Mkataba wa Dayton.
Mkataba huo wa amani uliigawa Bosnia katika eneo la Wa-Serbia, kwa jina la Jamhuri ya Srpska, na shirikisho la Waislamu na Wakroatia, kila upande ukiwa na serekali yake, bunge na polisi, kukiweko pia serekali kuu ilio dhaifu, wakiweko mawaziri watatu kutoka kila kundi.
Tamaa ya Bosnia ya kujiunga na Umoja wa Ulaya inategemea marekebisho yaliopendekezwa na Umoja wa Mataifa na kutajwa kuwa ni shuruti kabla ya nchi hiyo kutia saini mapatano ya kukaribiana na Umoja wa Ulaya wa nchi 27. Muhimu kati ya marekebisho hayo ni kuyaunganisha majeshi ya polisi. Jumapili iliopita, vyama sita muhimu vinavowaakilisha Wa-Serbia, Waislamu na wa-Kroatia viliahidi kuendelea kufanya mazungumzo kuhusu suala hilo.
Kwa jumla, Wa-Serbia wanapinga kuweko taasisi za serekali kuu zenye nguvu na wanashikilia kubakia na jeshi lao la polisi. Waislamu na Wakrotia, hata hivyo, wanataka majeshi mbali mbali ya nchi hiyo yaunganishwe. Wanasema chini ya mkataba wa Dayton, mabadiliko yeyote makubwa lazima yapate kibali cha pande zote za makabila hayo matatu.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Bwana Spiric alisema mfumo wa kuitawala Bosnia hauwezi kushikiliwa na jamii ya kimataifa, wakati yeye anatakiwa abebe dhamana. Aliongeza kusema kwamba uamuzi wake sio wazo la ghafla au umetokana na kuchokozwa. Alisema miaka 12 baada ya kutiwa saini mapatano ya Dayton, Bosnia-Herzegovina, kwa bahati mbaya, sio nchi huru; miaka kumi na mbili baada ya mapatano ya Dayton, wageni ndio pekee walio na usemi wa kuitawala nchi hiyo na anaamini jambo hilo sio zuri kwa nchi hiyo na wananchi wake. Alisema jamii yakimataifa ndio ilioipika supu hiyo, na sasa ni wakati ichukuwe kijiko na kuinywa.
Katika mahojiano wiki hii na Shirika la Habari la Kifaransa, AFP, waziri mkuu wa sehemu ya Wa-Serbia ya Bosnia, Milorad Dadik, alionya kwamba wabunge wa chama chake cha Social Democratic, SNSD, watajiuzulu kwa pamoja mnamo siku chache zijazo ikiwa Bwana Lajcak hatoyaondosha marekebisho alioyaanzisha. Chama cha SNSD ndicho kinachotawala katika upande wa Wa-Serbia katika ile inayoitwa Jamhuri ya Srpska. Lakini jana jamii ya kimataifa ilimuunga mkono Bwana Lajcak, ambaye ni mwanadiplomasia wa kutokea Slovakia. Baraza lenye dhamana ya kuyatekeleza mapatano ya Dayton lilisema hatua zilizochukuliwa na Bwana Lajcak kabisa zinaambatana na mamlaka yake na katiba.
Chini ya sheria huko Bosnia, rais lazima ateuwe mtu mwengine kuchukuwa nafasi ya waziri mkuu, na wadhifa wake lazima upewe kibali na bunge. Lakini wabunge wa Ki-Serbia huko Bosnia haifikiriwi kwamba watamuunga mkono mtetezi yeyote mpya kwa wadhifa huo. Hiyo ina maana nchi hiyo itakuwa haina serekali kwa kipindi kisichojulikana. Mapatano ya Dayton yanampa mwakilishi mkuu wa kimataifa mamlaka makubwa na ambayo hasa yanamruhusu kulazimisha sheria na kuwafukuza kazi maafisa waliochaguliwa ikiwa atawaona kuwa wanaweka vikwazo.