1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa China ziarani nchini Japan

Omar Babu12 Aprili 2007

Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, amekuwa kiongozi wa kwanza wa taifa lake kulihutubia bunge la Japan tangu miaka ishirini na miwili iliyopita. Wen Jiabao amewatolea mwito wabunge wa Japan daima wakumbuke uvamizi uliotekelezwa na nchi yao katika enzi ya vita vya pili vya dunia.

Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, akihutubia bunge la Japan.
Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, akihutubia bunge la Japan.Picha: AP

Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, yumo kwenye ziara ya siku tatu nchini Japan katika harakati ya kuurekebisha uhusiano uliozorota kati ya mataifa hayo mawili.

Kiongozi huyo wa China anazuru Japan wakati ambapo uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili unaelekea kuimarika.

Kwenye hotuba aliyotoa katika bunge la Japan, Wen Jiabao, amesisitiza kwamba nchi yake na pia Japan hazipaswi kuzingatia kupita kiasi matatizo ya kihistoria.

Mwelekeo wa uhusiano kati ya China na Japan umebadilika tangu msimu wa mapukutiko uliopita pale waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, alipoitembelea China.

Hilo lilidhihirika kinagaubaga kwenye hotuba ya Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, katika bunge la Japan.

Wen Jiabao alisema:

"Ikiwa ziara ya Shinzo Abe ya msimu wa mapukutiko iliuregeza mzizi wa fitna, basi ziara yangu mimi imeung`oa"

Waziri Mkuu Wen Jiabao ameungama kwamba watu wengi katika mataifa yote mawili waliathirika kwa kiasi kikubwa wakati wa vita.

Wen Jiabao ameelezea kuridhika na hatua ya Tokyo kuomba radhi kwa uvamizi wake dhidi ya China katika enzi ya vita vya pili vya dunia.

Kiongozi huyo wa China anazuru Japan kujaribu kuuimarisha uhusiano uliozorota katika utawala wa Waziri Mkuu wa zamani wa Japan, Junichiro Koizumi.

Mapema, Wen Jiabao, aliwatolea mwito wawekezaji wa Japan kuwa na imani na uchumi wa China, akisema kwamba serikali yake imepania kuthibiti ukuaji wake wa kiuchumi.

China ndiye mshirika mkuu wa kibiashara wa Japan.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyi biashara wa Japan wameilimbikizia lawama China wakisema ni hatarí kwa nchi hiyo kuwekeza kwa wingi bila kutilia maanani mataifa mengine.

Waziri Mkuu, Wen Jiabao, alishauriana na jumuiya ya wafanyi biashara wa Japan katika dhifa ya chakula cha mchana mjini Tokyo na kuihakikishia serikali yake imejitolea kurekebisha hali ya mambo.

Baadaye kiongozi huyo wa China aliungana na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, kufungua mkutano wa kiuchumi kati ya mawaziri wa kiuchumi wa nchi zao mbili.

Wen Jiabao ambaye ndiye kiongozi wa kwanza wa China kuitembelea Japan tangu miaka saba iliyopita, aliyataka mashirika ya Japan yawasaidie wafanyibiashara wa China kiufundi, hasa kuhusiana na nishati na pia jinsi ya kutunza mazingira.

Wachunguzi wa maswala ya kiuchumi wanatabiri yamkini ziara ya Waziri Mkuu Wen Jiabao nchini Japan ikaimarisha au kuongeza idadi ya wawekezaji wa kijapani nchini China.

Wachunguzi hao pia wanasema uhusiano kati ya mataifa hayo mawili utachukua mwelekeo mpya wenye hali ya kuaminiana.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW