1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Ethiopia aahidi mageuzi

Sekione Kitojo
2 Aprili 2018

Waziri mkuu mpya wa Ethiopia, Abiye Ahmed,ameahidi kusukuma mageuzi ya kidemokrasia katika juhudi za kufikisha  mwisho miaka mitatu ya ghasia zilizozuka kwanza katika jimbo la Oromiya ambako ndiko anakotokea.

Äthiopien Vereidigung Premierminister Abiy Ahmed
Picha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

Muungano unaotawala  nchi  hiyo  ulimteua Abiye wiki  iliyopita kuchukua  nafasi ya  Hailemariam Desalegn , ambaye  alijiuzulu  ili kusafisha  njia  kwa  ajili  ya  mageuzi nchini Ethiopia , nchi ya  pili yenye  wakaazi  wengi zaidi barani  Afrika  na  moja  kati ya  nchi zenye  uchumi  unaokua  kwa  haraka.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiye AhmedPicha: Reuters/Stinger

Baada  ya  kuapishwa , Luteni Jenerali  huyo  wa  zamani  wa  jeshi alizungumzia  kuhusu maridhiano  na  upinzani  lakini  hakutaja uwezekano wa  kuondoa  amri  ya  hali  ya  hatari  iliyodumu  kwa muda  wa  miezi  sita iliyowekwa  Februari mwaka  huu  baada  ya mtangulizi  wake  kujiuzulu.

"Leo  ni  siku  ya  kihistoria. Tunashuhudia  mabadilishano  ya madaraka kwa  njia  ya  amani. Leo  hali  yetu  inatuwekea  bayana fursa  na  vitisho," Abiye  aliwaambia  wabunge  katika  hotuba  ya dakika  40  iliyotangzwa  moja  kwa  moja  katika  televisheni.

"Demokrasia  haiwezi  kuwepo kunapokuwa  hakuna  haki,iwe haki za kiraia  ama  kiuchumi. Sisi  wote tunahitaji  jukwaa  la  kutoa  sauti zetu kwa  matatizo  yetu," aliuambia  mkusanyiko  huo, ambako baadhi  ya  wapinzani  pia  waliruhusiwa  kuhudhuria.

Jimbo  la Oromiya , ambalo  linazunguka   mji  mkuu  Addis Ababa , limekumbwa  na  ghasia  tangu  mwaka  2015, kwa  kiasi  kikubwa zikichochewa  na  hisia za  kutengwa  kisiasa na  kiuchumi miongoni mwa  vijana  wake.

Wabunge wa bunge la Ethiopia wakimkaribisha waziri mkuu mpya Abiye AhmedPicha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

Waoromo  ni  karibu  theluthi moja ya  Waethiopia  wote  nchini humo  wanaofikia  idadi  ya  watu  milioni  100.

Maandamano 

Chama  tawala  nchini Ethiopia  cha  Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kimekuwa  madarakani tangu mwaka  1991 , wakati  kilipochukua  madaraka  kutoka kwa utawala  wa  kijeshi  wa  Derg.

Maandamano  na  hali  ya  kutokuwa  na  utulivu  katika  jimbo  la Oromiya vimesababisha  kitisho  kikubwa  kuendelea  kutawala chama  hicho, na  hali  hiyo  imeongeza  wasi  wasi  wa  kikabila.

"Tuna historia  ndefu  kama  nchi. Lakini leo, uhusiano  baina  ya makundi  ya  kikabila umeharibika," alisema Seid Yimer , mwanasiasa  kutoka  katika  kabila  la  Oromo.

"Hilo  ni  lazima  liwe  kipaumbe kwake. Anapaswa  kuleta uhusiano mwema. Anapaswa  kuvunja sheria  ambazo zinachochea  tofauti," alisema, akimaanisha  mfumo  wa  Ethiopia  wa  majimbo   ambao uliunda  upya  mipaka  ya  majimbo  kwa  misingi  ya  kikabila wakati ilipotekelezwa  mwaka  1991.

Katika  hotuba  yake Abiye alizungumzia  haja  ya  umoja  wa kikabila.

Wabunge kutoka  Oromiya , kabila  kubwa  nchini  Ethiopia  kwa eneo  la  idadi  ya  watu , walikaribisha  uteuzi wa  kiongozi  kutoka katika  kabila  hilo  kubwa  ambalo  kwa  muda  mrefu  lilikuwa likilalamikia  kutengwa.

Waziri mkuu mpya wa Ethiopia Abiye Ahmed (kushoto) akiwa pamoja na mtangulizi wake Hailemariam Dessalegn wakishika bendera ya nchi hiyoPicha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

"Ni  mara  ya  kwanza  katika  historia  ya  Ethiopia  kwamba Muoromo amekuwa  kiongozi  wa  nchi  hiyo. Hii ni muhimu  sana kwasababu Waoromo  ni  wengi,"  alisema  mbunge  huyo Abera Buno.

Makundi  ya  haki  za  binadamu  yanasema  majeshi  ya  usalama yamewauwa  mamia ya  watu  na  kuwafunga  mamia  kwa  maelfu katika  miaka  mitatu  iliyopita.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW