1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ethiopia aizuru Eritrea

Daniel Gakuba
8 Julai 2018

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amewasili nchini Eritrea, kukutana na rais wa nchi hiyo Isaias Afwerki katika mazungumzo yanayolenga kurejesha mahusiano baina ya nchi hizo ambazo zimekuwa na uhasama wa miongo miwili.

Äthiopischer Ministerpräsident Abiy Ahmed beim Staatsbesuch in Eritrea
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed (kushoto) baada ya kupokelewa na Rais Isaias Afwerki mjini AsmaraPicha: Twitter/@fitsumaregaa

  

Kwenye uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, Waziri Mkuu Abiy amepokelewa na Rais Afwerki, huku wakikumbatiana na kuangua kicheko. Kuwasili kwake kumeonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya taifa ya Eritrea. Kundi kubwa la watu lilikuwa kando likiimba na kucheza huku wakivalia fulana zenye picha za viongozi hao wawili.

Ziara hii inafanyika mwezi mmoja baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuwashangaza wengi, alipoamua kuyatambua kikamilifu makubaliano yaliyomaliza vita vya mpaka baina ya nchi hizo ndugu, ambavyo vilidumu kwa miaka miwili. Ethiopia na Eritrea zimekuwa hazana uhusiano wa kidiplomasia tangu kuanza kwa vita hivyo mwaka 1998. Abiy mwenyewe alipigana katika mojawapo ya miji ambayo imekuwa kiini cha mzozo kati ya nchi hizo.

Juhudi za amani ya kudumu

Fitsum Arega ambaye ni kiongozi wa ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia, amesema kupitia mtandao wake wa twitter kwamba ziara ya Waziri Mkuu Abiy ina ''malengo ya kuimarisha juhudi za kufikia amani ya kudumu'' katika ya nchi hizo za Upemba wa Afrika.

Abiy na Afwerki wanaazimia kurejesha mahusiano baina ya nchi zaoPicha: Twitter/@fitsumaregaa

''Mataifa yetu mawili yana historia moja, na yanafungamana kwa namna ambayo siyo rahisi kuipata mahali pengine'' amesema Fitsum, na kuongeza kuwa huu unaweza kuwa mwanzo wa kumaliza miongo miwili ya kukoseana imani, na kuchukua mtazamo mpya.

Balozi wa Eritrea nchini Japan Estifanos Afworki, amesema, yeye pia kupitia mtandao wa twitter, kwamba hakuna kiongozi yeyote mwingine aliyepokelewa kwa furaha mjini Asmara kama Abiy Ahmed.

Upendo usio kifani

Waethiopia walioandamana na waziri wao mkuu katika ziara hii nchini Ethiopia, wameelezea kushtushwa na mapenzi waliyoonyeshwa. Mmoja wao amesema ilikuwa kama ndoto.

Kutambua makubaliano ya kumaliza vita na Eritrea ulikuwa uamuzi mkubwa zaidi miongoni mwa hatua nyingi za mageuzi alizozichukuwa Waziri Mkuu Abiy tangu kuingia madarakani Aprili mwaka huu. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 42 tayari amewaachia waandishi wa habari na wapinzani kutoka gerezani, na ameufungua uchumi wa nchi hiyo ambao kwa sehemu kubwa umekuwa ukidhibitiwa na serikali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape.rtre

Mhariri: John Juma

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW