1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Waziri Mkuu wa Haiti kuondoka Ijumaa

Josephat Charo
12 Machi 2024

Ariel Henry amekubali kujiuzulu huku magenge yenye silaha yakiitumbukiza nchi katika machafuko.

Waziri Mkuu anayeondoka wa Haiti Ariel Henry (kushoto) akiwa na waziri wa mamabo ya nje wa Marekani Antony Blinken  jijini NewYork
Waziri Mkuu anayeondoka wa Haiti Ariel Henry (kushoto) akiwa na waziri wa mamabo ya nje wa Marekani Antony Blinken jijini NewYorkPicha: Bing Guan/AP Photo/picture alliance

Katika hotuba ya kujiuzulu kwake aliyoichapisha kwenye mtandao, Henry amesema serikali anayoiongoza haiwezi kubaki katika hali ya kutojali na hakuna kujitolea kokote kunakoshinda taifa la Haiti.

"Haiti inahitaji amani. Haiti inahitaji uthabiti. Haiti inahitaji maendeleo endelevu. Haiti inahitaji kuzijenga upya taasisi zake za kidemokrasia.", alisema Henry.

Mataifa ya eneo la Caribbean yamefanikiwa kumshawishi kiongozi huyo ajiuzulu katika mkutano wa dharura mjini Kingston, Jamaica ambako waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alitoa dola milioni 100 kukifungulia njia kikosi cha ulinzi kitakachoongozwa na Kenya. Blinken ambaye alitumia muda wa saa saba katika mazungumzo ya Kingston amethibitisha kujiuzulu kwa Henry.

Afisa wa Marekani anayesafiri na Blinken amesema Henry amekubali kuondoka Ijumaa lakini anasubiri mkutano wa Kingston utoe maelekezo kuhusu kipindi hicho cha mpito.