1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Hungary asema kura ya bunge ni kisasi tu!

12 Septemba 2018

Wabunge wa bunge la Ulaya wamepitisha azimio la kuchukuliwa hatua za kuiadhibu Hungary kutokana na nchi hiyo kukiuka utawala wa sheria katika zoezi la kupiga kura katika bunge la Ulaya mjini Strasbourg.

EU-Parlament für Sanktionsverfahren gegen Ungarn
Picha: Reuters/V. Kessler

Wabunge hao wa bunge la Ulaya wameupitisha mchakato wa kuchukuliwa hatua za nidhamu dhidi ya Hungary kwa kupiga kura 448 dhidi ya kura 197 kati ya jumla ya kura 693 zilizopigwa. Wajumbe 48 hawakushiriki katika zoezi hilo la kupiga kura.

Hungary imesema kura ya bunge la Ulaya juu ya kuiadhibu serikali ya kizalendo ya nchi hiyo ni hatua ya kulipiza kisasi. Hata hivyo matokeo ya kura hiyo ni pigo kubwa kwa kwa waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban. Wabunge wa Ulaya wamepiga kura hiyo ili kuichukulia hatua Hungary kwa kikiuka maadili ya Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya nje wa Hungary Peter Szijjarto amesema uamuzi uliopitishwa leo na bunge la Ulaya ni hatua ya kulipiza kisasi ya wanasiasa wanaounga mkono sera ya uhamiaji. Waziri huyo aliitoa kauli hiyo muda mfupi tu baada ya bunge hilo kupiga kura hiyo inayoweza kuwa na maana ya Hungary kuwekewa vikwazo visivyokuwa na kifani. Matokeo ya kura hiyo yanaonyesha kuongezeka kwa mshikamano miongoni mwa vyama vya jadi barani Ulaya vinavyopinga kuongezeka kwa kasi ushawishi wa vyama vya mrengo mkali wa kulia vinavyopinga uhamiaji na ambavyo vinalaumiwa kwa kuudhoofisha utawala wa sheria.

Waziri mkuu wa Hungary Viktor OrbanPicha: picture-alliance/AP Photo/J.-F. Badias

Kura ya leo imeonyesha kwamba bunge la Ulaya kwa mara ya kwanza limeanza kuzitumia sheria zilizo chini ya ibara ya saba ya mkataba wa Umoja wa Ulaya. unayojulikana na wengine huko mjini Brussels kama "chaguo la nyuklia", ambalo linaweza kuiondolea Hungary haki za kupiga kura katika Umoja wa Ulaya.

Mbunge wa bunge la Ulaya wa chama cha Kijani cha Uholanzi Judith Sargentini, ambaye aliongoza upinzani dhidi ya waziori mkuu wa Hungary katika kura ya leo alionekana akitabasamu na kupumua kwa furaha kabla ya kuwakumbatia wafuasi wake kwenye bunge hilo la Ulaya katika mji wa Ufaransa wa Strasbourg.

Sargentini aliwaambia waandishi wa habari kwamba ni ishara nzuri inayoonyesha kuwa bunge hili linachukua jukumu lake na linataka hatua zichukuliwe.

Alikuwa amewahimiza wenzake wasiache kuiadhibu Hungary kwa sababu utawala wa Orban unakiuka maadili ambayo yanaujenga muungano wa Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya nje wa Hungary Peter SzijjartoPicha: Reuters/B. Szabo

Kura hiyo ilizingatia ripoti kuhusu wasiwasi juu ya uhuru wa mahakama, rushwa, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kitaaluma, uhuru wa kidini, na haki za wachache na wakimbizi chini ya utawala wa Orban katika muda wa miaka minane. Serikali nyingine za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinaweza kusimamisha hatua yoyote zaidi, hata hivyo, na Poland imeonya itaweza kufanya hivyo.

Katika hotuba yake fupi waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban alisema kwamba nchi yake itapinga hatua yoyote ya kutka kuishinikiza ilegeze msimamo wake wa kuwachukia wahamiaji akidai kuwa kura hiyo ilikuwa imepangwa hususan kuupendelea upande wa pili.

Orban amesema Hungary italinda mipaka yake, itapambana na uhamiaji haramu na itatetea haki yake. Orban ana mtazamo wa Ulaya ya Ukristo na anapinga wimbi la Waislamu na wahamiaji wengine wanaokuja barani Ulaya. Lakini Orban hapingwi tu na upande unaolemea mrengo wa kushoto bali anapingwa pia na wabunge wa upande wa kati kulia wa chama cha EPP.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW