1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatuhumiwa kuvuka mstari mwekundu

28 Septemba 2021

Israel yatoa onyo kwamba haitoikalia kimya Iran kuhusu kile ilichokiita juhudi za Iran za kutengeneza bomu la Nyuklia

Israels Ministerpräsident Naftali Bennett
Picha: Abir Sultan/AP/picture alliance

Waziri mkuu wa Israel Naftali Bennett ameishambulia Iran mbele ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa akisema nchi hiyo imevuka mipaka yote mnyekundu  iliyowekwa kwa lengo la kuizuia nchi hiyo kutoendelea na mpango wake wa kutengeneza silaha za Nyuklia.

Iran imekiuka mipaka yote iliyowekwa kuizuia kutengeneza silaha za Nyuklia,lakini Israel haitokubali kuiruhusu Tehran  kutengeneza bomu. Katika hotuba yake ya kwanza mbele ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa,tangu kuchukua nafasi ya waziri mkuu nchini Israel Naftali Bennett amesema Jamhuri ya kiislamu ya Iran katika miaka ya karibuni imezidi kuongeza urutubishaji madini ya Urani.

"Katika kipindi cha miaka michache iliyopita,Iran imepiga hatua kubwa kuendeleza mpango wake wa kutengeneza silaha za Nyuklia,katika urutubishaji wa madini ya urani.Mpango wa kutengeneza silaha za Nyuklia wa Iran umefikia mahala hatari. mipaka yote miyekundu imekwishavukwa,ukaguzi umepuuzwa,yote yaliyotakiwa kufanyika yameshindikana.Hivi sasa Iran inakiuka makubaliano ya kiusalama ya IAEA na haichukuliwi hatua.Inawanyanyasa wakaguzi na kuhujumu uchunguzi wao na haichukuliwi hatua.''

Picha: Fatemeh Bahrami/AA/picture alliance

Bennett amesema wapo watu duniani ambao wanaoiona hatua ya Iran ya kutaka kutengeneza silaha za Nyuklia kwamba haiwezi kuepukika au wameshachoka kusikia kuhusu suala hilo,lakini Israel haiwezi kudiriki kuchoka na haiwezi kuruhusu asilani Iran itengeneze silaha za Nyuklia.

Lakini Iran imemjibu kiongozi huyo wa Israel kwa kusema alichokionesha waziri mkuu Bennet ni kutaka kuonekana muhanga na amejaribu kwa inda kuuonesha ulimwengu kwamba utawala wa Israel hauna makosa.

Payman Ghadirkhomi, Naibu katibu wa ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameliambia baraza kuu la Umoja huo kwamba hatua ya waziri mkuu wa Israel sio kitu kingine bali undumilakuwili wenye lengo la kuyaondoa macho ya walimwengu kutotazama kitisho halisi kilichopo kwenye amani na usalama wa kikanda unaosababishwa na utawala wa Israel na hususan kuhusiana na zana zake za Nyuklia na mitambo yake isiyokuwa salama ya nyuklia pamoja na shughuli zake.

Picha: Ronald Zak/AP Photo/picture alliance

Marekani na Umoja wa Ulaya nazo pia jana ziliitolea mwito Iran kuruhusu wakaguzi kuingia kwenye eneo la  vinu vyake vya Nyuklia wakati Iran ikisema kwamba eneo hilo sio miongoni mwa maeneo yaliyojumuishwa kwenye ukaguzi kwa mujibu wa makubaliano ya hivi karibuni na shirika la kudhibiti nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA.

Naftali Bennett hajawahi kutamka kwa uwazi hadharani kuhusu mtazamo wake juu ya kufufuliwa kwa mpango wa kimataifa juu ya Nyuklia ya Iran lakini amemksoa mtangulizi wake Benjamin Netanyahu kwa kile alichokiita,mwanya ulioachwa kati ya kauli misimamo mikali  za viongozi waliopita juu ya Iran na uhalisia ulivyo. Iran ilitangaza wiki iliyopita kwamba inataraji kuona mazungumzo juu ya kufufuliwa tena makubaliano ya mwaka 2015 yanaanza tena na nchi hiyo kuondolewa vikwazo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/afpe

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW