1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaItaly

Waziri Mkuu wa Italia, Meloni, ajikuta mtegoni kwenye simu

Sylvia Mwehozi
3 Novemba 2023

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni imeelezea masikitiko yake baada ya kiongozi huyo kujikuta mtegoni na kuwa muhanga wa mawasiliano ya simu za mzaha!

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia MeloniPicha: Thomas Coex/AFP/Getty Images

Mawasiliano hayo yalimshawishi kutoa maoni yake kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine na kusikika akikiri kwa uwazi kwamba amechoshwa na vita hivyo. 

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni akiamini kuwa alikuwa akizungumza na maafisa wa Umoja wa Afrika, lakini badala yake yalikuwa ni mazungumzo baina yake na wachekeshaji wawili wa Urusi ambao hupiga simu za kufanya mzaha.

Alipoulizwa kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine, kiongozi huyo alisikika akisema kwamba "kuna uchovu mwingi sana, ningependa kusema ukweli. Tumekaribia wakati ambapo kila mtu anaelewa kuwa tunahitaji njia ya kutoka". Meloni anasikika zaidi akieleza kuwa "shida ni kutafuta njia ya kutoka ambayo inaweza kukubalika kwa pande zote mbili bila kuharibu sheria za kimataifa."

Serikali ya Meloni yatimiza mwaka mmoja madarakani

Matapeli Vovan na Lexus

Kipande hicho cha mawasiliano ya sauti ya simu ya Meloni na matapeli kilichapishwa siku ya Jumatano na vyombo vya habari vya Italia.

Matapeli hao pia wamewahadaa wanasiasa wengine wa nchi za Magharibi na watu mashuhuri katika jitihada za kutoa maoni yao ya wazi bila ya usalama.

Mawasiliano hayo ya simu yalifanywa na wasanii wa vichekesho wa Urusi Vovan na Lexus mnamo Septemba 18,  wakati wa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ambako Meloni alifanya mikutano na viongozi wa kiafrika.Picha: Imago Images/Russian Look/Interpress

Ofisi ya mshauri wa diplomasia ya Meloni imesema kuwa "inajutia kwa kupotoshwa na tapeli aliyejifanya kuwa rais wa halmashauri ya Umoja wa Afrika".

Waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani, alisema siku ya Alhamisi kwamba vipindi kama hivyo haviwezi kurudiwa. "Kwa hakika kulikuwa na ufundi wa hali ya juu kwa yeyote aliyepanga mawasiliano ya simu," Tajani aliiambia redio ya serikali ya RAI.

Meloni: Kuna ukosefu wa uungwaji mkono wa Italia

Katika kipande hicho cha sauti chenye dakika 13, mbali na kukiri kwamba mzozo wa Ukraine umeyachosha mataifa mengi, Meloni alieleza pia kwamba kumekuwa na ukosefu wa uungwaji mkono wa Italia katika kushughulikia mgogoro wa wahamiaji. 

Viongozi wa Afrika wataka kumaliza mzozo wa Ukraine

02:31

This browser does not support the video element.

Akisisitiza msimamo wa Italia kama nchi ya kwanza ambayo wahamiaji wengi wanaovuka bahari ya Mediterania hukimbilia, Meloni aliwalaumu washirika wa kimataifa kwamba hawafanyi vya kutosha kusaidia nchi hiyo.

"Wote wanakubali kwamba Italia  inapaswa kutatua tatizo hili peke yake. Ni njia ya kijinga sana ya kufikiri." Jamaa mmoja aliyeshiriki kupiga simu hiyo ya kuhadaa anayeitwa Lexus, alidai kwamba Meloni alikuwa tayari kutoa maoni yake ya kweli.

Alilieleza shirika la habari la Reuters kwamba "tofauti na viongozi wengine wa Ulaya wanakuwa kama maroboti na kutoa maoni ambayo yamekubalika miongoni mwa viongozi wenzao".

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW