Waziri mkuu wa Japan atangaza kujiuzulu.
2 Juni 2010Matangazo
Akizungumza na wabunge wa chama chake cha Democratic Party of Japan -DPJ-, katika kikao maalum kwenye bunge la nchi hiyo, Waziri Mkuu wa Japan Yukio Hatoyama alisema kwamba atajiuzulu, huku akitaka kuundwa upya kwa chama hicho. Amemtaka pia Katibu mkuu wa chama chake Ichiro Ozawa kujiuzulu na kusema kwamba Katibu Mkuu huyo amekubali ombo hilo. Kushuka kuungwa mkono kwa baraza lake la mawaziri kumekuja baada ya kuvunja ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, ya kuhamisha kituo cha jeshi la majini la Marekani kutoka katika kisiwa cha Okinawa. Waziri mkuu huyo pia anakabiliwa na shinikizo kubwa la kumtaka ajiuzulu kutoka katika chama chake cha Democratic Party of Japan -DPJ. Hatoyama ambaye amekuwa waziri mkuu wa nne wa Japan katika kipindi cha miaka minne aliuambia mkutano mkuu wa chama hicho kwamba anastaafu kwa sababu ya kujiondoa kwa chama cha Social Democratic SDP, katika serikali ya muungano. Chama hicho kilijiondoa siku ya Jumapili baada ya Hatoyama kuamua kuendelea kukiacha kituo cha jeshi la Marekani katika kisiwa kilichoko kusini mwa Japan. Uamuzi huo ulikuja baada ya Waziri mkuu Yukio Hatoyama kumfukuza siku ya Ijumaa kiongozi wa chama hicho cha Social Democratic Party -SDP- Mizuho Fukushima katika nafasi yake ya Waziri anayeshughulikia masuala ya jinsia, baada ya Bibi Fukushima kukataa kuidhinisha makubaliano juu ya kuhamishia makao mapya kituo hicho cha kijeshi cha Marekani. Chama tawala nchini Japan cha Democratic Party of Japan -DPJ- kinatarajia kufanya mkutano mkuu siku ya Ijumaa kuweza kuamua juu ya kiongozi mwingine ajaye. Chama hicho cha DPJ kina wabunge wengi katika bunge, ambalo ndio linachagua waziri mkuu. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wabunge wengi wa chama hicho cha Kidemokrasia cha DPJ, walipinga uchaguzi wa mwezi ujao wa bunge wakimtaka Waziri Mkuu huo kujiuzulu. Aidha baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa walionya kuwa chama hicho tawala kitashindwa katika uchaguzi kama hali haitabadilika. Upepo wa kisiasa uligeuka ghafla tofauti na wakati serikali hiyo mpya iliposhika madaraka ikiwa na umaarufu mwezi Septemba, baada ya chama cha DPJ kushinda kwa kishindo chaguzi mkuu wa mwezi Agusti mwaka jana. Kabla ya uchaguzi huo mkuu uliofanyika mwaka uliopita, Hatoyama aliahidi kuendeleza uhusiano ulio sawa na Marekani, nchi ambayo ni mshirika mkuu wa Japan, hujku akiwasisitizia wakazi wa kisiwa cha Okinawa kwamba hataruhusu kituo kingine cha kijeshio cha Marekani kujengwa katika kisiwa chao, lakini wiki iliyopita, serikali yake ilikubali ombi la Marekani kuhamishwa tena kituo katika eneo lisilo na watu wengi katika kisiwa hicho cha Okinawa licha ya upinzani uliokuwepo. Mwandishi: Halima Nyanza(dpa) Mhariri:Mtullya Abdu
Matangazo