1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amejiuzulu

12 Septemba 2007

Chama cha LDP nchini Japan kimepata pigo kubwa baada ya waziri mkuu kutangaza kuwa amejiuzulu kutoka kwenye wadhfa huo.

Bwana Shinzo Abe
Bwana Shinzo AbePicha: AP

Hatua hiyo imefuatia matokeo mabaya katika uchaguzi wa mwezi Julai ambapo chama chake cha Liberal Demokratik kilishindwa kupata kura za kutosha lakini bwana Abe aling’ang’ania madarakani kwa madai kwamba anataka kuendeleza mageuzi nchini Japan.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe aliejiuzulu anae tambulika kuwa ni mtu mwenye sifa ya moyo wa utaifa alipanda kwenye madaraka hayo mwaka uliopita lakini tangu pale chama chake cha Liberal Democratic kilipoangushwa katika uchaguzi wa bunge, alianza kukabiliwa na upinzani mkubwa na miito ya kumtaka ang’atuke madarakani.

Chama cha Liberal Democratic kilipoteza umaarufu wake kufuatia kashfa za fedha na akiba ya uzeeni ambazo ziliwakabili baadhi ya mawaziri katika serikali ya waziri mkuu Shinzo Abe.

Katibu wa baraza la mawaziri la Japan Kaoru Yosano ambae pia ni msemaji wa serikali ameashiria kuwa sababu za kiafya pia zimechangia kujiuzulu kwa waziri mkuu huyo mbali na joto la kisiasa.

Bwana Abe amesema kwa sasa ni vigumu kuendeleza sera ambazo zilidhaniwa kuwa zingeungwa mkono na kupata imani kubwa kutoka kwa raia wa Japan.

Na kwa ajili hiyo waziri mkuu huyo wakati wa kutangaza kujiuzulu kwake amesema kwamba wananchi wa Japan wanahitaji kiongozi walie na imani nae na pia wakatae muunga mkono.

Kujiuzulu kwa bwana Abe kumesababisha pigo kubwa katika chama chake cha LDP.

Wengi wanaamini kuwa mswaada wa bwana Abe wa kupambana na ugaidi huenda ukakosa kufaulu bungeni.

Bwana Abe alikabiliwa na wakati mgumu kuushawishi upande wa upinzani kuweza kumuunga mkono katika mpango wake wa mageuzi na pia kuongeza muda wa vikosi vya kijeshi vinavyo ongozwa na Marekani nchini Afghanistan.

Hata ingawa waziri mkuu Abe aliejiuzulu hakutaja hasa ni lini atakapo ondoka ofisini lakini tayari amekiagiza chama chake kuanza kumsaka mrithi wake.

Chama cha LDP kinatarajiwa kufanya uchaguzi wake tarehe 19 mwezi huu wa Septemba, kwa mujibu wa radio ya taifa nchini Japan ya NHK.

Huenda katibu mkuu wa chama cha LDP, Taro Aso au katibu wa baraza la waziri wa zamani Yasuo Fukuda ndio watakao pendekezwa kugombea wadhfa wa bwana Abe.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Party Of Japan ( DPJ) Ichiro Ozawa amesema kwamba atatumia ushawishi mkubwa wa chama chake bungeni kupinga kuungwa mkono mpango wa vikosi vinavyo ongozwa na Marekani nchini Afghanistan.

Sheria inayoruhusu kuwepo kikosi cha Japan nchini Afghnistan inamalizika muda wake mwezi Novemba mwaka huu na hivyo basi mvutano uliopo sasa nchini humo kuhusu mpango huo huenda ukailazimu Japan kusimamisha mchango wa kikosi chake nchini Afghanistan.

Marekani imeonya kwamba kuondoka kikosi cha Japan kutoka nchini Afghanistan kutaathiri uhusiano na ushirika wa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili.

Hali ya kisiasa nchini Japan iliathiri kwa muda mfupi thamani ya Yen dhidi ya Dola katika masoko ya hisa.