Waziri mkuu wa Japan ziarani mjini Berlin
5 Mei 2009Waziri mkuu wa Japan,Taro Aso yuko ziarani nchini Ujerumani.Hii ni ziara yake ya kwanza tangu alipokabidhiwa wadhifa huo mwezi September mwaka jana.
Ujerumani na Japan zimeweka kando mvutano wao wa hivi karibuni kuhusu namna ya kupambana na mgogoro wa kiuchumi ulimwenguni.Baada ya kuikosoa Ujerumani wakati wa mkutano wa kilele wa mataifa 20 mjini London,waziri mkuu wa Japan Taro Aso,akiitembelea kwa mara ya kwanza Ujerumani,amesifu hii leo hatua za serikali kuu ya mjini Berlin za za kukabiliana na mgogoro huo.
Baada ya mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel,waziri mkuu Taro Aso amesema mjini Berlin "Ujerumani imegutuka mapema."Japan inapanga nayo pia kuanzisha mpango kama ule wa serikali kuu ya mjini Berlin wa kuwalipa fidia wenye kumiliki magari makongwe ili kuwahimiza wanunue magari mepya.
Kansela Angela Merkel amesema nchi hizi mbili zinaweza kushikilia nafasi ya mbele katika juhudi za kuhifadhi hali ya hewa na kushirikiana zaidi katika kubuni na kueneza tenknolojia ya usafi wa mazingira.
Waziri mkuu huyo wa Japan aliikosoa vikali Ujerumani katika mkutano wa kilele wa G-20 mjini London,April mwaka huu kwa kupinga fedha zaidi zisitolewe kuinua shughuli za kiuchumi.
Akihutubia katika chuo kikuu cha Humbold mjini Berlin waziri mkuu Taro Aso ameshadidia umuhimu wa kushirikiana kwa dhati Japan na Ulaya katika wakati huu wa mgogoro mkubwa kabisa wa kiuchumi.Ili kukabiliana na mgogoro huo,serikali ya mjini Tokyo imeshatenga yuro bilioni 90 hadi sasa na inadhamiria kutoa yuro bilioni 112 za ziada ili kuunusuru uchumi wa nchi hiyo.
Kansela Angela Merkel amekumbusha Ujerumani inafanya mengi katika kuimarisha shughuli za kibiashara.
Hadi wakati huu Ujerumani imeshapitisha mipango miwili ya kuinua uchumi,yenye thamani ya yuro bilioni 80.Kutokana na kuongezeka malipo ya uzeeni na malipo ya wasiokua na ajira,Ujerumani kwa mujibu wa kundi la vyama ndugu vya CDU /CSU bungeni,inapanga kutoa yuro bilioni 200 za ziada kuinua shughuli za kiuchumi.
Viongozi hao wawili wamezungumzia hofu walizo nazo kutokana na hali namna ilivyo nchini Pakistan.Waziri mkuu Taro Aso amekumbusha nchi yake imeshaandaa mkutano wa wafadhili kwaajili ya Pakistan.
Japan ni miongoni mwa nchi zinazoathirika vibaya sana na mgogoro huu wa kiuchumi.
Baadae hii leo waziri mkuu wa Japan Taro Aso amepangiwa kuzungumza na rais wa Shirikisho Horst Köhler.
Mwandishi :Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Abdul Rahman