Waziri mkuu wa Kongo Lukonde ajiuzulu
21 Februari 2024Matangazo
Waziri mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jean-Michel Sama Lukonde amejiuzulu, hatua inayosababisha kuvunjwa serikali yake. Waziri mkuu huyo aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Felix Tshisekedi siku nane baada ya kuidhinishwa kwa nafasi yake kama mbunge wa kitaifa.
Sasa atahudumu bungeni katika nafasi ya ubunge. Ofisi ya rais imesema ombi lake la kujiuzulu limekubaliwa. Hata hivyo, rais ameiomba serikali ya Lukonde kuendelea kuyashughulikia masuala ya sasa hadi pale serikali mpya itakapoundwa.
Haikutoa sababu za kujiuzulu kwa waziri huyo mkuu. Lukonde aliteuliwa waziri mkuu wa nchi hiyo yenye utajiri wa madini Februari 2021. Alikuwa na umri wa miaka 43 wakati huo.