1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Hatma ya waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan mashakani

9 Aprili 2022

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan anakabiliwa na kura kali ya kutokuwa na imani naye Jumamosi iliyowasilishwa na wapinzani wake wa kisiasa, ambao wanasema wana kura za kumshinda.

Pakistan Politik I Imran Khan
Picha: Anjum Naveed/AP/picture alliance

Upinzani ulioungana na kujumlisha mirengo yote ya kisiasa kuanzia kushoto hadi msimamo mkali wa kidini unasema una kura 172 unazohitaji katika Bunge la Pakistan lenye viti 342 ili kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Imran Khan.  

Khan alitumia televisheni ya taifa siku ya mkesha wa kura kutoa wito kwa wafuasi wake kuingia mitaani kuandamana siku ya Jumapili, katika ishara kwamba aliamini angepoteza kura hiyo.

Soma pia: Wabunge Pakistan kuanza kupiga kura ya kutokuwa na imani na Khan

Mahakama ya Juu ya Pakistan yenye majaji watano siku ya Alhamisi ilizuia ombi la Khan kusalia madarakani, na kuamua kuwa hatua yake ya kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema haikuwa halali.

Uamuzi wa mahakama hiyo wa Alhamisi uliweka mazingira ya kupiga kura ya kutokuwa na imani naye, ambayo huenda ikamuendea kinyume Khan, baada ya wanachama wake kadhaa wa chama chake tawala na mshirika mdogo lakini muhimu wa muungano kuhamia upinzani.

Waziri Mkuu Imran Khan akihutubia wafuasi wake.Picha: Daniel Berehulak/Getty Images

Katika mazungumzo mafupi bungeni Jumamosi, kiongozi wa upinzani Shahbaz Sharif alionya dhidi ya ucheleweshaji zaidi wa kura hiyo. Sharif ndiye anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Khan iwapo Khan atapoteza kura hiyo, ambayo upinzani ulianzisha mwezi uliopita ukimtuhumu waziri mkuu huyo kwa usimamizi mbovu wa kiuchumi ambao umeongeza bei na viwango vya riba.

Miito ya uchunguzi kuhusu njama kati ya upinzani na Marekani

Waziri wa mambo ya nje wa Khan Shah Mahmood Qureshi, amedai uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya chama tawala kwamba kura hiyo ya kutokuwa na imani na waziri mkuu ni njama ya upinzani na Marekani kumng'oa Khan ambaye hakuwepo.

Soma pia:Imran kumwita Osama shahid ni kuteleza ulimi?

Qureshi alirejea hotuba yake kwa bunge majira ya mchana katika kile ambacho baadhi ya wabunge wa upinzani walisema ni mbinu ya kuchelewesha ya serikali.

Katika hotuba yake iliyojaa hisia siku ya Ijumaa, Khan alisisitiza shutuma zake kwamba wapinzani wake walishirikiana na Marekani kumng'oa kutokana na chaguo lake la sera za kigeni, ambazo mara nyingi zilionekana kupendelea China na Urusi na kukataa ukosoaji wa Marekani.

Khan alisema Washington ilipinga mkutano wake wa Februari 24 na Rais wa Urusi Vladimir Putin katika ikulu ya Kremlin saa chache baada ya vifaru vya Urusi kuingia Ukraine kuanzisha vita vikali katikati mwa Ulaya.

Waziri Mkuu Imran Khan akiwa katika mkutano na rais wa Urusi Vladmir Putin, siku Moscow ilipoanza uvamizi dhidi ya Ukraine.Picha: Mikhail Klimentyev/Sputnik/Getty Images/AFP

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imekanusha kuhusika kwa namna yoyote na siasa za ndani za Pakistan. Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Jalina Porter aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kuwa "hakuna ukweli kabisa kuhusu madai haya."

"Bila shaka, tunaendelea kufuatilia maendeleo haya na tunaunga mkono mchakato wa kikatiba wa Pakistan, lakini narudia tena, madai hayo hayana ukweli kabisa,'' alisema.

Soma pia: Chuki dhidi ya Uislamu: Imran Khan ajenga daraja kati ya mashariki na magahribi

Hata hivyo, Khan aliwataka wafuasi wake kuingia mitaani, hasa vijana ambao wamekuwa kundi kubwa linalomuunga mkono tangu nyota huyo wa zamani wa kriketi alipoingia madarakani mwaka wa 2018. Alisema wanahitaji kuipinga Marekani ambayo inataka kuiamrisha Pakistan ili kulinda uhuru wa Pakistan.

Imran Khan ajitangazia ushindi huko Pakistan

00:54

This browser does not support the video element.

"Lazima mjitokeze kulinda mustakabali wenu. Ni nyinyi mnaopaswa kulinda demokrasia yenu, mamlaka ya nchi yenu na uhuru wenu. ... Huu ni wajibu wenu,'' alisema. "Sitakubali serikali kibaraka."

Muungano usiotarajiwa

Njia za Khan ni chache na iwapo watu wengi watajitokeza kumuunga mkono, anaweza kujaribu kuendeleza kasi ya maandamano ya mitaani kama njia ya kushinikiza bunge livunjwe na kwenda kwenye chaguzi za mapema. Kupoteza kura ya kutokuwa na imani na Khan siku ya Jumamosi kutaleta mamlakani baadhi ya washirika wasiotarajiwa.

Miongoni mwao ni chama kikubwa cha kidini ambacho kinaendesha shule nyingi za kidini. Chama hicho cha Jamiat-e-ulema-Islam, au Baraza la Wahubiri, JUI, hufundisha aina ya Uislamu wa kihafidhina zaidi katika shule zake. Wengi wa Taliban wa Afghanistan na Taliban wa Pakistani walihitimu kutoka shule za JUI.

Washia wa Pakistan na wafuasi wa chama tawala cha Pakistan Tehreek-e-Insaf wakichoma bendera ya Marekani nje ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Lahore kupinga kile walichosema ni njama ya Marekani kumuondoa waziri mkuu Imran Khan. Picha: K.M. Chaudary/AP/picture alliance

Vikubwa zaidi miongoni mwa vyama vya upinzani, kile cha Pakistan People's Party, kinachoongozwa na mtoto wa aliyekuwa waziri mkuu aliyeuawa Benazir Bhutto, na Pakistan Muslim League, vimetiwa doa na madai ya ufisadi uliokithiri.

Kiongozi wa chama cha Pakistan Muslim League, na waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif, alipatikana na hatia ya ufisadi baada ya kutajwa katika kile kinachoitwa Nyaraka za Panama.

Huo ni mkusanyo wa nyaraka za siri za kifedha zilizovujishwa zinazoonyesha jinsi baadhi ya matajiri duniani wanavyoficha pesa zao na kuhusisha kampuni ya mawakili ya kimataifa iliyoko Panama. Sharif aliondolewa na mahakama ya juu ya Pakistan kushikilia wadhifa wake.

Ikiwa upinzani utashinda kura ya kutokuwa na imani naye, ni juu ya bunge kuchagua kiongozi mpya wa serikali, ambaye anaweza kuwa ndugu wa Sharif, Shahbaz Sharif. Ikiwa wabunge hawatafaulu, uchaguzi wa mapema utaitishwa.

Chanzo: APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW