1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Sudan arejeshwa nyumbani

27 Oktoba 2021

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amerejeshwa nyumbani jana usiku, baada ya siku ya shinikizo kubwa la kimataifa kufuatia kuondolewa kwake katika mapinduzi ya kijeshi.

Sudan | nach Putschversuch | Premierminister Abdalla Hamdok
Picha: AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amerejeshwa nyumbani jana usiku, baada ya siku ya shinikizo kubwa la kimataifa kufuatia kuondolewa kwake katika mapinduzi ya kijeshi. Ofisi yake imesema Hamdok amewekwa chini ya uangalizi wa karibu wakati mawaziri wengine na viongozi wa kiraia wakisalia chini ya kifungo cha nyumbani.

Soma pia: Jeshi la Sudan: Tulimkamata waziri mkuu kwa usalama wake

Marekani ilisema itasitisha msaada wa kifedha kuhusiana na mapinduzi hayo na Umoja wa Ulaya ukatishia kuchukua hatua sawa na hiyo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura kujadili hali ya Sudan huku tamko la pamoja likitarajiwa kutolewa leo.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alichukua madarakaPicha: Sudan TV/AP/picture alliance

Awali, Jenerali mkuu Abdel Fattah al-Burhan alisema Hamdok anashikiliwa nyumbani kwa jenerali huyo na yuko katika afya nzuri. Raia waliokuwa waliingia mitaani kupinga mapinduzi hayo. Watu wanane waliuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama kwa mujibu wa duru za hospitali.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametetea hatua ya jeshi kutwaa madaraka kwamba ilikuwa ya lazima ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe. Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu alipotangaza kudhibiti madaraka, al-Burhan amewashutumu wanasiasa kwa uchochezi dhidi ya vikosi vya usalama.

Soma pia: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuijadili Sudan

Amedai kwamba Hamdok anashikiliwa nyumbani kwake na hajadhurika hata kidogo. Kiongozi huyo wa kijeshi anasema kitendo hicho cha jeshi hakiwezi kuhesabiwa kama mapinduzi kwasababu jeshi lilikuwa likijaribu kurekebisha njia ya kipindi cha mpito cha kisiasa.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW