Mariano Rajoy ameshindwa katika kura ya kutokuwa na imani
1 Juni 2018Sanchez alishinda kwa kura 180 dhidi ya 169 zilizopinga na moja kujizuwia kupiga kura.
Rajoy ameondolewa madarakani kutoka na kashfa ya ufisadi iliyokikumba chama chake cha Popular Party PP ambapo maafisa wa zamani wameshitakiwa kwa kuchukua rushwa ili kutoa kandarasi.
Kabla ya kura kupigwa Rajoy aliliambia bunge la nchi hiyo kuwa anajivunia rekodi yake kama waziri mkuu wa taifa hilo, akimpongeza mpinzani wake Sanchez na wabunge wa chama tawala cha Popular Party- PP wakimpigia makofi na kusimama kumuonesha heshima zao.
Rajoy alisema ilikuwa ni fahari kwake kuiacha Uhispania katika hali nzuri kuliko alivyoikuta na kuwashukuru Wahispania na kuwatakia kila la kheri.
"Imekuwa ni fahari kuwa Waziri Mkuu wa Uhispania. Ni fahari kuweza kuondoka na kuacha Uhispania kuwa bora kuliko jinsi nilivoipata."
Sanchez hatakubali Catolonia kujitenga
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Kisosholisti Pedro Sanchez aliliambia bunge kabla ya matokeo kwamba leo wanaandika historia kuhusu demokrasia ya taifa hilo. Lakini mbunge wa chama cha PP Rafael Hanando amemwambia Sanchez kuwa atakuwa waziri mkuu wa Uhispania kupitia mlango wa nyuma kwasababu alishidwa katika uchaguzi mwaka 2015 na 2016.
Kuondoka kwa Rajoy baada ya miaka sita kama Waziri mkuu kutaliweka taifa hilo lenye uchumi wa nne kwa ukubwa katika Umoja wa Ulaya katika hali ya wasiwasi na kisiasa, Italia inapojikwamua kutoka kwenye mzozo.
Wawekezaji wengi hawaoni hatari ya kuwekeza nchini Uhispania kama ilivyo Italia kwani Sanchez mwenyewe anaiunga mkono Ulaya ambapo viongozi wengi wa vyama vya miungano wameibua masuala kuhusu nia zao za kuunga mkono sarafu ya euro.
Vyama viwili vinavyounga mkono uhuru wa Catalonia pamoja na kile cha mrengo wa kushoto cha Podemos pia vilisema tangu awali vitamuunga mkono Sanchez. Sanchez ameahidi kuanzisha mazungumzo na Wakatolonia, lakini akasema hatuwapa nafasi ya kujitenga.
Baada ya kura Sanchez anatarajiwa kuapishwa wikendi hii na kuteua baraza lake la mawaziri. Hata hivyo akiwa na viti 84 kati ya 350 vya bunge, serikali yake itakuwa na wakati mgumu wa kupitisha sheria.
Uchaguzi mkuu wa Uhispania umepangwa kufanyika katikati ya mwaka 2020 na haijabainika iwapo Sanchez ataitisha uchaguzi mkuu wa mapema kabla ya wakati.
Wadadisi wengi wanasema kuwa huenda akasubiri hadi kufanyika kwa uchaguzi wa Ulaya, wa mitaa na wa majimbo mwezi Mei mwaka ujao.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, Reuters, Dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman