Waziri Mkuu wa Uhispania Sanchez ziarani Ukraine
1 Julai 2023Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez yuko katika mji mkuu wa Ukraine Kyiv kwa mazungumzo na Rais Volodymyr Zelensky. Sanchez aliwasili Kyiv mapema leo ikiwa ni siku ya kwanza ya Uhispania kukalia kiti cha urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Ukraine kupokea bilioni dola 1.5 kusaidia kujijenga upya
Waziri Mkuu huyo wa Uhispania amesema baada ya kuwasili Kyiv kuwa alitaka kitendo cha kwanza cha urais wa Uhispania katika Umoja wa Ulaya uanze kwa pamoja na Zelensky.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuwasilisha kwa Ukraine ujumbe kuwa Ulaya itaendelea kuwa na mshikamano na nchi hiyo iliyovamiwa.
Sanchez amesema kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kuwaunga mkono watu wa Ukraine hadi amani irejee Ulaya. Hii ni ziara ya tatu ya Sanchez mjini Kyiv tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine Februari 2022.