1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Uingereza arejea kazini

Admin.WagnerD27 Aprili 2020

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Uingereza imeanza kupata mafanikio kwenye mapambano yake dhidi ya virusi vya corona lakini ameashiria vizuizi vikali vilivyowekwa havitoondolewa hivi karibuni. 

Großbritannien Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris JohnsonPicha: picture-alliance/dpa/S. Rousseau

Waziri Mkuu Johnson amesema hayo wakati alipolihutubia taifa kwa mara ya kwanza kiasi mwezi mmoja tangu alipoambukizwa virusi vya corona na kulazimika kulazwa hospitali ikiwemo siku kadhaa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Akizungumza nje ya ofisi yake iliyoko mtaa wa Downing mjini London, Johnson ameufananisha ugonjwa wa COVID-19 kuwa sawa na mhalifu anayekwapua mitaani ambaye raia wa Uingereza wamefanikiwa kumshinda nguvu na kumdhibiti.

Johnson amesisitiza licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kuvishinda virusi vya corona, bado ni mapema mno kuondoa vizuizi vilivyopo na amewataka raia waUingereza kuonesha mshikamano zaidi kama uliooneshwa katika kipindi cha wiki sita zilizopita.

Uingereza ni moja ya mataifa yaliyoathiriwa vibaya na virusi vya corona na hadi siku ya Jumamosi  imerikodi zaidi ya vifo vya watu 20,000.

Tangu nchi hiyo ilipotangaza viuzuizi vikali vilivyojumuisha kuzuia watu kutoka nje isipokuwa kwa sababu muhimu, serikali ya Johnson imekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka vyama vya upinzani na baadhi ya madaktari kwa kuchelewa kuweka marufuku, uwezo mdogo wa kufanya vipimo na ukosefu wa vifaa muhimu.

Mataifa mengine yaendelea kulegeza vizuizi

Picha: Getty Images/J. Lago

Hayo yanajiri wakati mataifa mengine barani Ulaya yanachukua hatua za polepole kulegeza viuzizi vilivyowekwa kudhibiti kuenea virusi vya corona ambavyo vimewakumba kiasi watu milioni 3.

Jana Jumapili watoto nchini Uhispania  waliruhusiwa kwa mara ya kwanza kutoka nje baada ya muda wa wiki sita.

Chini ya kanuni mpya, watoto wanaruhusiwa kujumuika na wengine kati ya saa tatu asubuhi hadi saa tisa mchana, lakini hawaruhusiwi kwenda umbali za ya mita 700 kutoka yalipo makaazi yao.

Kwa upande wake, Italia imetangaza kuwa shule zitafunguliwa tena mwezi Septemba lakini biashara nyingi zitaanza tena kazi wiki inayokuja.
Ufaransa inatazamiwa kuweka mpango wake wa kufungua tena shughuli za uchumi kesho Jumanne.

Gates amsifu Kansela Merkel 

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Katika hatua nyingine, mfanyabiashara tajiri Bill Gate amemsifu kansela wa Ujerumani Angela Merkal kwa jinsi alivyoishughulikia kadhia ya virusi vya corona.

Bill Gates ameliambia gazeti la Frankfurter Allgemeine kuwa Bibi Merkel ni kiongozi wa mfano na ishara ya wazi ya jinsi ugonjwa wa COVID-19 unavyopaswa kushughulikiwa.

Kwengineko, Saudi Arabia imesema itaondoa kwa sehemu fulani marufuku yake ya saa 24 kwa kuruhusu baadhi ya maduka makubwa na biashara za rejareja kufungua tena shughuli zake.

Lakini taifa hilo imesititiza hatua hiyo haitaugusa mji mtukufu wa Makka utakaoendelea kuwa chini ya vizuizi vikali vya kuzuia watu kutoka nje.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW