Waziri Mkuu wa Uingereza awasili Ukraine
12 Januari 2024Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak yuko ziarani nchini Ukraine kuzindua awamu mpya ya msaada kwa ajili ya Ukraine na kuongeza ufadhili wa kijeshi kwa mwaka huu wa fedha hadi pauni bilioni 2.5.
Ofisi ya Sunak imesema fedha hizo ni ongezeko la pauni milioni 200 katika kipindi cha miaka miwili, na itahakikisha dhamira kubwa zaidi kuwahi kutokea ya kuipatia droni serikali ya Ukraine.
Soma pia:Sunak: Uingereza itasimama kidete na Ukraine
Sunak pia anatarajiwa kusaini makubaliano ya kihistoria ya ushirikiano wa usalama na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky. Ufadhili huo wa ziada utajumuisha manunuzi ya makombora ya masafa marefu, mfumo wa ulinzi wa anga, na usalama baharini.
Waziri huyo mkuu wa Uingereza pia anatarajiwa kukutana na wafanyakazi wa huduma za dharura ambao wanatoa huduma baada ya mashambulizi ya anga ya Urusi.