1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss ajiuzulu

20 Oktoba 2022

Liz Truss ambaye amekuwa ofisini kwa wiki sita pekee, ametangaza kujiuzulu kwake kama Waziri Mkuu wa Uingereza.

UK London | Rücktritt Liz Truss
Picha: Alberto Pezzali/AP Photo/picture alliance

Kwenye hotuba yake ya kujiuzulu Alhamisi mbele ya ofisi yake, Liz Truss amekiri kuwa asingeweza kutimiza ahadi alizotoa alipokuwa akiwania wadhifa wa kuwa kiongozi mkuu wa chama cha Conservative kumwezesha kuwa Waziri Mkuu.

Kujiuzulu kwake kumetokana na mpango wake wa kiuchumi uliosababisha mtikisiko wa masoko ya kifedha na kukigawa chama chake, wiki sita tu tangu alipochukua wadhifa huo.

Uingereza: Mivutano yazidi kuudidimiza uongozi wa Waziri Mkuu Liz Truss

"Natambua kwamba kutokana na hali hii, siwezi kutimiza jukumu nililopewa na chama cha Conservative. Hivyo nimezungumza na mtukufu Mfalme kumuarifu kwamba najiuzulu kama kiongozi wa chama cha Conservative. Asubuhi hii nimekutana na mwenyekiti wa kamati ya 1922, Graham Brady, tumekubaliana kwamba kutakuwepo na uchaguzi wa kiongozi utakaokamilishwa wiki ijayo. Nitasalia kuwa waziri Mkuu hadi mrithi wangu atakapochaguliwa," amesema Truss.

Mapema Alhamisi waziri mwengine katika baraza lake aliwasilisha barua ya kutokuwa na inami na serikali ya Liz Truss.

Jumatano jioni, waziri wa mambo ya ndani aliyejiuzulu, Suella Braverman alikuwa waziri wa pili kuondoka katika baraza la mawaziri la Waziri Mkuu Liz Truss.

Zaidi ya dazeni moja ya wabunge wa Conservative walitamka hadharani Truss ajiuzulu, na wengine zaidi waliripotiwa kuwasilisha barua kwa Brady wakitaka aondolewe, ingawa sheria za chama zimepiga marufuku kampeni nyingine ya uongozi kwa muda wa miezi 12. 

Awali Truss aliomba radhi kutokana na mpango wake uliozusha mtikisiko, lakini alisema katu hatang'atuka.

Waziri Mkuu mpya anatarajiwa kuteuliwa wiki ijayo. 

Kiongozi wa upinzani Uingereza Keir Starmer ataka uchaguzi mkuu ufanywe kufuatia hatua ya Liz truss kujiuzulu kama Waziri Mkuu.Picha: Stefan Rousseau/dpa/picture alliance

Chama cha Labour chaitisha uchaguzi mkuu

Hata hivyo kiongozi wa upinzani Keir Starmer ambaye chama chake cha Labour kimeshuhudia uungwaji wake mkono ukiongezeka pakubwa katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura kufuatia muhula mfupi wa Truss uliokumbwa na mzozo, ametaka uchaguzi mkuu uitishwe sasa.

"Tuko tayari kuunda serikali ili kutuliza uchumi na kutekeleza mpango halisi wa ukuaji, wa kuboresha viwango vya maisha, kusaidia watu kuvuka mzozo wa gharama za maisha. Na hilo ndiyo chaguo sasa: Seriakli imara au vurugu hizi kutoka kwa Wahafidhina," amesema Starmer.

Truss alichukua wadhifa huo baada ya Boris Johnson ambaye pia alilazimika kujiuzulu.

Sarafu ya Uingereza yaanguka dhidi ya dola
Kinyang'anyiro cha kumchagua mrithi wa Truss

Mwenyekiti wa Kamati ya wabunge wa Conservative inayohusika na uchaguzi wa viongozi Grahma Brady, ametangaza kinyang'anyiro cha kumchagua mrithi wa Truss kitafanyika kufikia Oktoba 28. Miongoni mwa wanaopigiwa upatu kuwania nafasi hiyo ni pamoja na waziri wa sasa wa fedha Jeremy Hunt, Rishi Sunak na hata mtangulizi wa Truss, Boris Johnson.

Maoni: Namna ufalme wa Uingereza unavyoilinda nchi dhidi ya kusambaratika

Madhila ya waziri Mkuu huyo yalianza wakati mpango wake wa kupunguza kodi, uliposababisha sokomoko kwenye masoko ya fedha ambalo lilitishia mifuko ya pensheni, na kumlaazimisha kufanya mabadiliko kadhaa ya kufedhesha.

Kuondoka kwa Braverman jana, kulisababisha mabadiliko ya pili ya baraza la mawaziri mwezi huu, baada ya hapo awali Truss kumfuta kazi mshirika wa karibu Kwasi Kwarteng kuhusiana na vurumai la bajeti, na nafasi yake kujazwa na Jeremy Hunt, ambaye mara moja alifuta karibu matangazo yote ya kisera.