1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Uingereza yuko ziarani China

28 Januari 2026

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer anaanza ziara ya siku tatu nchini China leo Jumatano.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer anasaka ushirikiano wa kibiashara katika ziara yake nchini China.Picha: Suzanne Plunkett/AP Photo/picture alliance

Kiongozi huyo anatumai kuwashawishi watawala mjini Beijing kuwa serikali mjini London inatafuta ushirikiano madhubuti hata baada ya miaka kadhaa ya mahusiano yaliyotetereka.

Ziara hiyo inafanyika wakati ambapo Uingereza inapitia misuguano ya kidiplomasia na mshirika wake wa karibu, Marekani.

Akiwa mjini Beijing, Waziri Mkuu wa Uingereza, Kier Starmer, atakutana baadae leo na Rais Xi Jinping wa China na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Li Qiang.

Ziara hiyo ni kwanza kufanywa na kiongozi wa Uingereza nchini China tangu mwaka 2018 na Starmer anatumai atamudu kuitumia kuimarisha mahusiano yanayosuasua baina ya nchi hizo mbili.

Waziri mkuu huyo ameambatana na ujumbe mkubwa wafanyabiashara pamoja na mawaziri wawili.

Moja ya ajenda kubwa ya Starmer, ni kutafuta ushirikiano kati ya Uingereza na China kwenye sekta za teknolojia na kuzinadi bidhaa za Uingereza kwenye soko la China ikiwemo magari na mvinyo kutoka Scotland.

China na Uingereza zinatafuta mashirikiano ya "vitendo badala ya maneno"

Rais Xi Jinping wa China.Picha: Greg Baker/AFP/Getty Images

Pande zote mbili zimesisitiza kwamba suala muhimu kushinda yote katika kuimarisha tena mahusiano ni, "kutekeleza kwa vitendo yote yatakayoafikiwa badala ya maneno matupu."

Katika wakati Rais Donald Trump anaitikisa misingi ya ushirikiano wa kimataifa iliyoasisiwa na Marekani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, serikali mjini London na Beijing zinasaka mahusiano madhubuti yatakayotuama juu ya biashra na ushirikiano kwenye maeneo mfano wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Starmer aliliambia Baraza lake la Mawaziri jana Jumanne kabla ya kuelekea China, kuwa Uingereza iliupa kisogo uhusiano wake na China lakini serikali yake inataka mashirikiano na dola hiyo yenye uchumi wa pili wa ukubwa duniani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa China, Guo Jiakun, amesema ziara ya Starmer itakuwa nafasi ya kukuza imani ya kisiasa na ushirikiano madhubuti baina ya nchi hizo mbili chini ya kiwingu cha kile amekitaja kuwa "hali isiyotabirika ulimwenguni".

Beijing itamudu kuiamini Uingereza baada ya miaka ya msukosuko?

Mivutano kati ya Trump na viongozi washirika wa nchi za magharibi inatazamiwa huenda itaimairisha nafasi ya China kimataifa. Picha: The Presidential Office of Ukraine/Captital Pictures/picture alliance

Hata hivyo China itampokea Starmer kwa tahadhari kwa sababu ya historia ya sera isiyo thabiti ya Uingereza kuelekea Beijing.

Mahusiano ya nchi hizo yamepwaya miaka ya karibuni licha ya tangazo la kuanza kwa "enzi ya dhahabu" ya ushirikiano lililotolewa mwaka 2015 na serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, David Cameroon.

Warithi wa Cameroon hawakuyapa umuhimu mahusiano ya Uingereza na China wakitoa sababu za ukaribu wa Beijing na Urusi, tuhuma kwamba China ilikuwainafanya ushushushu na udukuzi hasa wa kiuchumi na rikodi dhaifu ya haki za binadamu hususani kwenye jiji la Hong Kong.

Ziara ya Starmer inafanyika huku mipasuko ikianza kuonekana kati ya Uingereza na mshirika wake mkuu wa Marekani. Vitisho vya ushuru, shinikizo la Trump kutaka kukichukua kisiwa cha Greenland na madai yake kuwa washirika wa Jumuiya ya NATO hawatajitokeza kuisaidia Marekani, vyote hivyo vimeongeza mafuta kwenye moto.

Utawala wa Trump bila shaka utakuwa unaifuatilia kwa karibu ziara ya Starmer mjini Beijng na dalili zote kwamba Uingereza itaijongelea sana China, yumkini zitaikasirisha Washington.

Wakati wa ziara hiyo Starmer atautembelea pia mji mkubwa wa kibiashara wa Shanghai kabla ya baadae kuelekea nchini Japan.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW