1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila Amolo Odinga aaga dunia akiwa na miaka 80

15 Oktoba 2025

Waziri Mkuu wa zamani Kenya Raila Odinga, kiungo muhimu katika siasa za Afrika ameaga dunia kutokana na mashituko wa moyo akiwa na umri wa miaka 80. Raila umauti umemkuta nchini India alikokuwa anapokea matibabu.

Raila Odinga kiongozi wa chama cha ODM
Waziri Mkuu wa zamani Kenya Raila Odinga aaga dunia nchini India akiwa na umri wa miaka 80Picha: Jessica Rinaldi/REUTERS

Raila Odinga aliaga dunia akiwa katika hospitali ya Devamatha nchini India katika jimbo la Kerala. Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya aliyewahi kugombea urais wa taifa hilo mara tano kwa zaidi ya miongo mitatu, alitia saini mwezi Machi mwaka huu, mkataba wa kisiasa na rais wa Kenya William Ruto, kama ishara ya azma yao ya kushirikiana kwenye serikali moja.

Mkataba huo ulihimiza mshikamano wa kisiasa na utawala unaojali usawa na fursa kwa wote.

Nafasi hiyo ilifungua mlango wa chama chake cha upinzani kuhusishwa katika maamuzi ya sera muhimu za serikali na hata baadhi ya wanachama wake kuteuliwa kushika nafasi muhimu katika Baraza la Mawaziri. 

Odinga amekuwa sauti kubwa ya demokrasia, mabadiliko,haki na diplomasia ya kikanda. Hivi karibuni alishindwa katika uchaguzi wa kuwa mwenyekiti wa Halmashauri Kuu  ya Umoja wa Afrika. 

Rais Ruto kulihutubia taifa kuhusu kifo cha Raila

Rais wa Kenya Wiiliam Ruto anatarajiwa kulihutubia taifa kuhusu kifo cha ´Mwasiasa huyo mashuhuri barani Afrika, Raila Odinga. 

Kabla ya taarifa za kifo chake kuthibitishwa, kulikuwa na uvumi mtandaoni kwamba alikuwa tayari ameshafariki, lakini familia yake ilikanusha na kusema anachangamoto za kiafya lakini yuko salama.

Kifo cha Raila Odinga ni pigo kubwa kwa siasa za Kenya na ukanda wa Afrika Mashariki.

Rais wa Kenya William Ruto Picha: Shisia Wasilwa/DW

Alijulikana kwa msimamo wake thabiti kuhusu demokrasia, haki za binadamu, na mageuzi ya kitaifa, na alibeba matumaini ya mamilioni ya Wakenya waliotamani mabadiliko ya kisiasa.

Viongozi wa Afrika na dunia wamuomboleza Raila

Viongozi mbali mbali wa Afrika na dunia wanaendelea kutoa salamu zao za rambirambi kwa wakenya na familia kwa kuondokewa na kiongozi huyo muhimu, aliyenyoosha siasa za taifa hilo. Rais wa Zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema taifa limempoteza mtu muhimu aliyejenga amani na demokrasia yaKenya.

Nae Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika AU Mahmood Ali Youssouf, amesema Raila alikuwa mtu muhimu katika siasa za Kenya, shujaa wa demokrasia, utawala bora na maendeleo. Ameongeza kuwa Afrika imempoteza kiungo muhimu wa kisiasa.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa upande wake amesema Kenya na Afrika kwa ujumla,  imempoteza kiongozi mahiri, mpenda amani na mtafuta suluhu ambaye ushawishi wa upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa Ujumla wake. 

Kiongozi mwengine aliyechangia pia kutoa pole kwa wakenya wakati taifa likiomboleza ni Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, aliyesema amesikitishwa na kifo cha rafiki yake Raila Odinga.  Amesema Raila alikuwa rafiki wa dhati wa watu wa India na kwamba  alipenda sana dawa za kiasili za India zilizokuwa na matokeo chanya kwa afya ya mtoto wake wa kike. 

Raila Odinga alizaliwa Januari 7, 1945. Alikuwa mtoto wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga. Alirithi si tu jina la familia lenye uzito wa kisiasa, bali pia moyo usiyotetereka wa kupigania haki.