1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa zamani Thailand adaiwa kutoroka

25 Agosti 2017

Yingluck Shinawatra, huenda akawa ameikimbia nchi yake siku chache baada ya kesi ya ufisadi dhidi yake kusomwa kwenye Mahakama Kuu, na sasa haijulikani hatima ya Waziri huyo mkuu wa zamani.

Thailand Yingluck Shinawatra
Picha: Getty Images/AFP/L. Suwanrumpha

Siku chache baada ya Mahakama Kuu ya Thailand kutoa amri ya kukamatwa kwa aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, Yingluck Shinawatra, vyanzo vya habari nchini humo vimeeleza kuwa ameondoka na huenda amekimbilia Singapore.

Shinawatra ambaye anatoka katika familia iliyoteka siasa za Thailand kwa zaidi ya miaka 15 anadaiwa kuondoka nchini humo baada ya kushindwa kuonekana mahakamani Ijumaa.

Mwanasiasa huyo alikuwa akisomewa mashtaka ya uzembe katika utoaji wa zabuni ya ununuzi wa pembejeo za kilimo cha mpunga, kitendo kilichosababisha hasara ya zaidi ya mabilioni ya dola.

Naibu Waziri Mkuu wa Thailand, Prawit Wongsuwan, amewaambia wanahabari kuwa inawezekana Shinawatra ametoroka.

"Tunaendela kuchunguza kama kweli ametoroka. Wanausalama wetu wa kimataifa hawawezi kuruhusu hilo. Tunakagua mipaka yote. Kama kuna ripoti yoyote kuwa ametoroka kupitia kisiwa hicho cha Chnga, tutazifanyia kazi".

Baadaye aliwaambia wanahabari hao kuwa polisi wanachunguza taarifa za waziri huyo wa zamani zinazoeleza kuwa amekimbilia kisiwa cha Koh Chang, kilicho karibu na mpaka wa Cambodia. Hata hivyo polisi nchini Cambodia wamesema hajaingia nchini humo.

Mahakama ilitoa amri ya kukamatwa kwake na kutupilia mbali ombi la wakili wa Shinawatra aliyedai kuwa mteja wake anaumwa na hivyo angeshindwa kuhudhuria mahakamani.

Picha: Reuters/J. Silva

Akitoa amri ya kukamatwa kwake, Jaji Kiongozi Cheeü Chulamon aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo itasikilizwa tena Septemba 27.

Endapo atapatikana na hatia kutokana na makosa hayo ya uzembe, huenda akafungwa miaka 10 jela na kuzuiwa kujihusisha na siasa katika maisha yake yote.

Waziri wa zamani wa biashara katika serikali yake alihukumiwa kifungo cha miaka 42 jela kutokana na makosa yanayofanana na ya Shinawatra.

Maofisa usalama nchini humo wamesema hawajui alipokimbilia waziri huyo lakini wametoa amri ya mipaka yote kukaguliwa kwa umakini.

Kiongozi mkubwa wa chama cha Shinawatra, aliiambia AFP kuwa mwanasiasa huyo ameondoka na huenda  amekimbilia Singapore.

 Profesa wa masuala ya siasa nchini humo, Puangthong Pawakapan anasema huenda huu ukawa mwisho wa maisha ya kisiasa kwa familia ya Shinawatra, ambaye kaka yake pia aliwahi kuwa waziri mkuu wa taifa hilo.

" Nadhani matokeo ya haraka kwa sasa ni mwisho wa familia ya Shinawatra katika siasa, kwa sababu ndugu wawili wameshakosa sifa za kuingia katika siasa tena na sidhani kama atakuwepo mwanafamilia mwingine kuongoza chama hicho. Na kuhusu chama cha Pheu Thai Party, nadhani kitasambaratika”

Wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa mahakamani, mamia ya wafuasi wake walikusanyika nje ya mahakama  wakimsubiri kiongozi huyo, wengine wakiwa wameshika maua na baadhi walionekana wakiwa wamevaa glovu nyeupe zilizoandikwa neno ‘upendo'.  Hata hivyo polisi zaidi ya 4,000 walitanda katika eneo hilo.

Wakati huo huo, Shinawatra ameandika katika ukurasa wake Facebook jana akiwataka wafuasi wake kukaa nyumbani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuwaathiri au kuiathiri nchi.

Kaka yake Shinawatra, aliondolewa madarakani na jeshi mwaka 2006  na akakimbilia ughaibuni akikwepa mashtaka ya rushwa.

Mwandishi: Florence Majani/dpa/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef