1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mpinzani mkuu wa Hasina aachiliwa huru Bangladesh

Angela Mdungu
6 Agosti 2024

Baada ya rais wa Bangladesh Mohammed Shahabuddin kulivunja bunge, Ofisi yake imetangaza kuwa imemuachia huru aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa chama cha upinzani cha BNP, Begum Khaleda Zia

Khaleda Zia ameachiliwa huru siku moja baada ya Sheikh Hasina kujiuzulu
Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh, Begum Khaleda Zia Picha: A.M. Ahad/picture alliance/AP Photo

Hatua hiyo ni mfululizo wa matukio yanayoendelea baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu na kukimbilia uhamishoni kutokana na maandamano yaliyodumu kwa karibu mwezi mmoja.

Begum Khaleda Zia, mwenyekiti wa Chama cha BNP ambaye amekuwa mpinzani mkuu wa Sheikh Hasina kwa miongo kadhaa, amewekwa huru kutoka katika kifungo cha nyumbani alichokuwa akikitumikia. Awali, Zia alihukumiwa kutumikia kifungo hicho jela kwa makosa ya rushwa mnamo mwaka 2018. Alianza kutumikia kifungo cha nje kutokana na sababu za kiutu mwaka 2022 baada ya serikali kusitisha kifungo chake gerezani.

Soma zaidi: Nguvu ya vijana yaanguasha utawala wa miaka 15 Bangladesh

Taarifa ya ofisi ya rais kuhusu kuachiliwa kwake imesema pia kuwa mchakato wa kuwaachilia wafungwa wengine wa kisiasa wakiwemo watu waliokamatwa wakati wa vuguvugu la wanafunzi la kupinga ubaguzi katika mgawanyo wa nafasi za kazi tayari umeanza.

Hayo yanajiri muda mfupi baada ya Rais Mohammed Shahabuddin kulivunja bunge. Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari  na ofisi ya Rais uamuzi wa kulivunja bunge umefikiwa baada majadiliano na wakuu wa utumishi wa jeshi, viongozi wa vyama vya siasa, wawakilishi wa asasi za kiraia na viongozi wa wanafunzi walioanzisha maandamano.

Soma zaidi: Wanafunzi wapendekeza mshindi wa Nobel kuwa Waziri Mkuu Bangladesh

Mapema leo, kiongozi wa wanafunzi walioanzisha maandamano yaliyosababisha Waziri Mkuu Hasina ajiuzulu, Nahid Islam alitangaza kuwa vuguvugu hilo limempendekeza mshindi wa tuzo ya Nobel Muhammad Yunus aongoze serikali ya mpito.  

Waandamanaji wakisherehekea kujiuzulu kwa waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina 05.08.2024Picha: Piyas Biswas/SOPA Images/Sipa USA/picture alliance

Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wahofia mashambulizi dhidi ya baadhi ya makundi Bangladesh

Katika hatua nyingine, wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya nchini Bangladesh wamesema wana hofu kuhusu uwepo wa ripoti za mashambulizi dhidi ya ya makundi ya walio wachache. Ni baada ya taarifa kuwa, baadhi ya biashara na makazi ya Wahindu, wanaoonekana kama kundi lililokuwa na ukaribu na Hasina walishambuliwa Jumatatu.

Ofisi za chama cha Sheikh Hasina Awami League kote nchini humo nazo zilichomwa moto kwa mujibu wa watu walioshuhudia. China kwa upande wake imesema inafuatilia hali ya yanayojiri Dhaka na inatumai Bangladesh itarejesha utulivu.

Zaidi ya watu 300 waliuwawa na wengine maelfu walijeruhiwa nchini humo, kutokana na maandamano yaliyotawaliwa na vurugu nchini humo yaliyoanza tangu mwanzoni mwa mwezi Julai.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW