1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Khan wa Pakistan afunguliwa mashitaka ya ugaidi

22 Agosti 2022

Polisi nchini Pakistan imefunguwa mashitaka ya ugaidi dhidi ya waziri mkuu wa zamani, Imran Khan, hatua inayozidi kuchochea mivutano kwenye taifa hilo lililotumbukia kwenye mzozo wa kisiasa tangu kuondolewa madarakani.

Pakistan | Imran Khan
Picha: K.M. Chaudary/AP Photo/picture alliance

Mashitaka hayo ya ugaidi yanahusiana na hotuba aliyoitowa Khan mjini Islamabad siku ya Jumamosi, ambapo aliapa kwamba angeliwashitaki maafisa wa polisi na jaji mmoja wa kike, akituhumu kwamba msaidizi wake wa karibu amekuwa akiteswa mikononi mwa vyombo vya dola tangu akamatwe. 

Mwenyewe Khan hakuzungumzia hati ya mashitaka yaliyofunguliwa dhidi yake na polisi, lakini chama chake - Tahreek-e-Insaf - kilisambaza picha mtandaoni zinazoonesha maelfu ya wafuasi wake wakiizunguka nyumba yake kuwazuwia polisi kumfikia.

Maoni:Pakistan inaelekea wapi baada ya kuondolewa kwa Khan ?

This browser does not support the audio element.

Aliyekuwa waziri wa habari kwenye serikali ya Khan, Fawad Chaudhry, alisema wafuasi hao waliendelea kusalia kwenye eneo hili tangu asubuhi ya Jumatatu, licha ya polisi kutoonesha hadi sasa jaribio la kumkamata.

Chaudhry alichapisha picha ikimuonesha Khan akifanya mkutano akiwa nyumbani kwake asubuhi ya leo.

Chama chake kimetishia kuitisha maandamano nchi nzima endapo kiongozi wao huyo atakamatwa.

Khan asaka dhamana ya kutokamatwa

Sehemu ya wafuasi wa Imran Khan waliozunguka nyumbani kwake kumlinda asikamatwe na polisi siku ya Jumatatu (Agosti 22, 2022).Picha: Anjum Naveed/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, wakili wa Khan, Bawar Awan, amefunguwa maombi kwenye Mahakama Kuu ya Islamabad, akitaka dhamana ya kumlinda waziri mkuu huyo wa zamani asikamatwe. 

Kwa mujibu wa sheria za Pakistan, polisi hufungua kile kiitwacho taarifa ya awali kuhusiana na mashitaka dhidi ya mshukiwa kwa mahakama ya mwanzo, ambayo nayo huruhusu uchunguzi kuendelea. Hapo ndipo polisi wanapoweza kumkamata na kumuhoji mshukiwa.

Taarifa hiyo ya awali dhidi ya Imran Khan inajumuisha ushahidi wa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Ali Javed, ambaye anasema alikuwapo kwenye mkutano wa hadhara mjini Islamabad siku ya Jumamosi na kumsikia Khan akimkosowa mkuu wa jeshi la polisi na jaji mwengine. Ushahidi huo unamnukuu Khan akisema: "Nanyi pia jitayarisheni, tutawachukulia hatua. Nyinyi musiokuwa na haya."

Uwezekano wa kifungo

Sehemu ya wafuasi wa Imran Khan waliozunguka nyumbani kwake kumlinda asikamatwe na polisi siku ya Jumatatu (Agosti 22, 2022).Picha: Anjum Naveed/AP Photo/picture alliance

Khan anaweza kukabiliwa na kifungo cha miaka kadhaa jela kutokana na mashitaka haya mapya chini ya sheria ya uchochezi, iliyorithiwa kutoka serikali ya kikoloni ya Muingereza. 

Hata hivyo, hajawahi kuwekwa kizuizini hata mara moja kwa mashitaka mengine madogo madogo ambayo amekuwa akifunguliwa mara kwa mara tangu aanze kampeni yake dhidi ya serikali.

Waziri Mkuu wa sasa wa Pakistan, Shahbaz Sharif, anatarajiwa kujadiliana na wenzake serikalini juu ya mashitaka dhidi ya Khan katika mkutano wa baraza la mawaziri uliopangwa kufanyika siku ya Jumanne (Agosti 23).

Mahakama nchini Pakistan inatuhumiwa kwa kuwa na historia ya kutumika kisiasa na kuegemea upande mmoja dhidi ya mwengine pale nchi inapokuwa kwenye vita vya kuwania madaraka baina ya jeshi, serikali ya kiraia na wanasiasa wa upinzani, kwa mujibu wa taasisi ya kupigania demokrasia duniani, Freedom House, yenye makao yake makuu jijini Washington, Marekani.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW