1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Imran Khan ahukumiwa miaka 3 jela

Angela Mdungu
5 Agosti 2023

Mahakama ya Islamabad imemhukumu Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan miaka mitatu jela. Ni baada ya kumkuta na hatia katika kesi ya rushwa iliyokuwa inamkabili.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Imran KhanPicha: Akhtar Soomro/REUTERS

Wataalamu wa masuala ya sheria wanasema huenda hukumu hiyo ikafifisha uwezekano wa Khan kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika kabla ya mwezi Novemba.

Chama cha siasa cha Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) katika kauli yake kimesema tayari kimeshaomba kukata rufaa katika mahakama ya juu. Vyombo vya habari vya Pakistan na shirika la habari la Reuters viliripoti juu ya uwepo wa polisi walioyazunguka makazi ya waziri mkuu huyo wa zamani mjini Lahore kabla ya hukumu kusomwa ambapo sasa tayari ameshakamatwa.

Khan mwenye miaka 70, aliyewahi kuwa mchezaji wa kriketi, alikuwa anatuhumiwa kwa kuuza na kununua zawadi za nchi alizopewa wakazi wa ziara zake katika mataifa ya nje. Zawadi hizo zina thamani ya zaidi ya rupia milioni 140 za Pakistani sawa na dola za Kimarekani 635,000. Khan mwenyewe amekanusha tuhuma hizo

Khan akiondoka mahakamani Juni 7, 2023Picha: K.M. Chaudary/AP/picture alliance

Hii ni mara ya pili kwa Imran Khan kukamatwa mwaka huu. Hukumu ya wakati huenda huu ni pigo la kisiasa kwa Khan na huenda ikasababisha asishiriki tena siasa. Waziri mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alipendekeza bunge livunjwe Agosti 9 kabla ya muda wake kwisha, na hivyo kutoa mwanya kwa uchaguzi mkuu kufanyika mwezi Novemba.

Msururu wa kesi za Khan

Tangu alipoondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye bungeni Aprili 2022, ameshitakiwa katika zaidi ya kesi 150 yakiwemo mashtaka kadhaa ya rushwa, ugaidi na kuwachochea watu wafanye vurugu wakati wa maandamano ya mwezi Mei.

Kukamatwa kwa Khan na kushikiliwa kwake mwezi Mei katika kesi nyingine tofauti kulisababisha mtikisiko wa kisiasa na machafuko makubwa yaliyotokea kati ya wafuasi wake na polisi. 

Kwenye maandamano hayo wafuasi wake walivamia mali za jeshi na serikali kote nchini Pakistan. Hukumu iliyotolewa dhidi ya Khan  inahofiwa kuwa huenda ikachochea machafuko mapya nchini humo wakati ambapo wengi wa wafuasi wake bado wana kesi kutokana na machafuko ya Mei.

Polisi wakiondoka kwenye makazi ya Khan mjini Lahore baada ya kumkamataPicha: Arif Ali/AFP

Soma zaidi: Pakistan: Waziri mkuu wa zamani Imran Khan awekezwa kizuizi cha kusafiri nje ya nchi

Chama cha waziri huyo mkuu wa zamani wa Pakistan kimehoji kuhusu mwenendo wa kesi wakidai kwamba mashahidi hawakupewa nafasi na muda wa kutosha wa kufanya majumuisho ya hoja zao, Waziri wa habari wa Pakistan Marriyum Aurangzeb ameviambia vyombo vya habari kuwa Khan amekamatwa baada ya taratibu kufuatwa.

Kwa mujibu wa Aurangzeb, katika kesi hiyo iliyosikilizwa zaidi ya mara 40, Khan alihudhuria mara tatu pekee. Amesema serikali haikutumia mkono wake dhidi ya Imran Khan kama yeye alivyokuwa akifanya dhidi ya upinzani wakati wa utawala wake. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW