Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto anatarajiwa kuzikwa leo baada ya swala ya Ijumaa.
28 Desemba 2007Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan aliyeuwawa Benazir Bhutto atazikwa karibu na kaburi la baba yake katika eneo la asili yake kusini mwa jimbo la Sindh baada ya swala ya Ijumaa leo.
Mazishi yatafanyika kiasi cha saa nane mchana saa za huko Pakistan katika kijiji cha Garhi Buksh, amesema kepteni Wasif Syed, kiongozi mwandamizi wa chama cha Pakistan Peoples Party PPP ambacho bibi Bhutto alikuwa akikiongoza.
Atazikwa karibu na kaburi la baba yake mzazi Zulfiqar Ali Bhutto katika makaburi ya familia katika kijiji hicho baada ya swala ya Ijumaa.
Maelfu kadha ya watu wameanza kujikusanya kwa ajili ya mazishi , amesema Syed, huku akibubujikwa na machozi.
Katika moja ya hotuba zake katika mikutano ya hadhara bibi Bhutto aliwashambulia wale wenye imani kali na wapiganaji kwa kusema kuwa nchi hiyo inapaswa kupambana nao.
Baadhi ya watu wanasema kuwa kauli yake ya kutaka kupambana na wapiganaji wenye imani kali ndio sababu ya kushambuliwa mara kwa mara na hatimaye kuuwawa hapo jana. Lakini aliyekuwa mshauri wa karibu wa bibi Bhutto katika mahojiano na shirika la utangazaji la CNN amesema kuwa serikali ya Pakistan huenda pia inahusika sana na kifo cha kiongozi huyo mashuhuri wa upinzani nchini Pakistan.
Ghasia zilizuka nchini Pakistan leo wakati watu wenye hasira wafuasi wa kiongozi huyo wa upinzani Benazir Bhutto walipoingia mitaani siku moja baada ya kuuwawa katika shambulio la kujitoa muhanga, wamesema watu walioshuhudia pamoja na polisi.
Polisi katika eneo linalomilikiwa na India la Kashmir wamepambana leo na mamia ya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe , wakipinga kuuwawa kwa kiongozi huyo wa upinzani nchini Pakistan Benazir Bhutto.
Majeshi ya usalama katika mji ulioko upande wa kusini wa Karachi wameamriwa leo kuwapiga risasi watu watakaofanya ghasia popote watakapowaona ili kuzuwia ghasia.Meja Athar Ali amewaambia waandishi wa habari kuwa wanajeshi wamepewa amri ya kuwapiga risasi iwapo wataona watu wakijihusisha na vitendo dhidi ya serikali, wakishambulia mali za serikali ama kuchoma moto mali za watu binafsi. Mitaa ya Karachi, mji mkuu wa jimbo la Sindh na mji mkubwa zaidi nchini Pakistan , ilikuwa haina watu leo Ijumaa huku maduka yakiwa yameharibiwa na majeshi ya ulinzi pamoja na polisi wakiwa wanafanya doria mitaani.
Tangu jana uharibifu mkubwa umefanyika . Maduka , magari na majengo ya serikali yamechomwa moto, amesema afisa mwandamizi wa polisi mjini Karachi Azhar Ali Farooqi.