Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan afungwa jela kwa ufisadi
17 Januari 2025Hukumu hiyo imetolewa Ijumaa na Jaji Nasir Javed Rana katika mahakama ya kupinga ufisadi iiliyoanzishwa kwenye gereza la Adiala, Rawalpindi, ambako Khan amefungwa tangu Agosti, mwaka 2023.
Bibi ambaye ni mke wa Khan, alishtakiwa Februari, mwaka 2024 na alikuwa nje kwa dhamana, lakini alikamatwa baada ya hukumu hiyo kutolewa.
Bibi ahukumiwa kwa kumsaidia mumewe
Mwendesha mashtaka Muzaffar Abbasi, amesema Bibi amekutwa na hatia ya kumsaidia mumewe kufanya uhalifu huo.
Khan na mkewe wanatuhumiwa kwa kukubali zawadi ya kipande cha ardhi iliyotolewa na mfanyabiashara wa mali zisizohamishika Malik Riaz, kama hongo wakati Khan alipokuwa waziri mkuu wa Pakistan.
Khan, mwenye umri wa miaka 72 na aliyeondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye Aprili, mwaka 2022, amekanusha madai hayo akisema analengwa na wapinzani wake kisiasa ili kumzuia asigombee uchaguzi. Mkewe pia amekanusha madai hayo.
Waziri wa Sheria wa Pakistan, Azam Nazeer Tarar amewaambia waandishi habari kuwa chama cha Khan kinaweza kuwasilisha rufaa ya kupinga hukumu hiyo kwenye mahakama za juu, na kwamba nyota huyo wa zamani wa mchezo wa kriketi anaweza pia kuwasilisha maombi ya kusamehewa kwa rais wa Pakistan.
Khan: Sitofikia makubaliano yoyote
Hata hivyo, akizungumza na waandishi habari baada ya hukumu kutolewa, Khan amesema hatofikia makubaliano yoyote, wala kuwasilisha ombi la msamaha.
Aidha, Omar Ayub msaidizi wa Khan, amesema chama chake kitaipinga hukumu hiyo kwenye mahakama za juu. Faisal Chaudhry, wakili wa Khan amesema kesi ya mteja wake imechochewa kisiasa na kwamba watakata rufaa katika mahakama ya juu.
Siku ya Alhamisi, Waziri wa Habari wa Pakistan, Attaullah Tarar aliwaambia waandishi habari mjini Islamabad kuwa kuna ''ushahidi usioweza kukanushwa'' dhidi ya Khan na mkewe katika kashfa hiyo kubwa ya ufisadi. Kulingana na Tarar, Khan hata hakulijulisha baraza lake la mawaziri kuhusu fedha ambazo zilirudishwa Pakistan na Uingereza.
Tuhuma za kurejesha fedha kwa mfanyabiashara
Khan anatuhumiwa kurejesha pauni milioni 90 kwa tajiri Riaz, baada ya fedha hizo kugunduliwa na kurejeshwa na Shirika la Uhalifu la Uingereza, kufuatia madai kwamba mfanyabiashara huyo alizipata kwa njia ya kutakatisha fedha. Pesa hizo zilipaswa kutolewa kwa taifa la Pakistan.
Waendesha mashtaka wamesema kama malipo ya kurejeshewa pesa hizo, mfanyabiashara huyo aliwapatia Khan na mkewe mali kadhaa za kibiashara na makaazi kupitia shirika lisilo la kiserikali la hisani la Al-Qadir, ambalo walilianzisha wakati Khan yuko madarakani.
Khan alikuwa waziri mkuu wa Pakistan kati ya mwaka 2018 na 2022.
(AFP, AP, Reuters)