Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan yuko katika "hali nzuri"
8 Agosti 2023Msemaji wa Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan amesema Imran Khan yupo katika hali nzuri licha ya kuwa katika mazingira magumu gerezani.
Khan, alikamatwa siku ya Jumamosi baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya ufisadi na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Msemaji wa Khan Raoof Hasan amesema kiongozi huyo wa zamani anazuiliwa katika mazingira ya kusikitisha ambayo hayafai kwa binaadamu yeyote na kwamba Khan alimtuma awaambie watu wake kwamba kamwe hatoyumbishwa katika msimamo wake.
Wanasheria wanaomwakilisha wamekutana jana na Khan katika jela ya wilaya ya Attock takriban kilometa 60 magharibi mwa mji mkuu Islamabad, na kusema wameanza matayarisho ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo na kuwasilisha ombi la kutaka aachiwe kwa dhamana.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewatolea wito viongozi wa Pakistan kuheshimu utaratibu unaostahili na utawala wa sheria. Khan mwenye umri wa miaka 70, analituhumu jeshi na wapinzani wake kisiasa kwa kula njama dhidi yake kupitia njia za kisheria.