Waziri mkuu wa zamani wa Thailand ahamishiwa hospitali
23 Agosti 2023Waziri Mkuu wa zamani wa Thailand Thaksin Shinawatra amehamishiwa hospitali ya polisi kutoka gerezani mapema siku ya Jumatano, ikiwa ni chini ya siku moja baada ya kurejea nchini kutokea uhamishoni na kuanza kutumikia kifungo chake cha miaka nane.
Thaksin mwenye umri wa miaka 74, aliwekwa jela ili kutumikia vifungo kutokana na hukumu za makosa kadhaa ya uhalifu zilizotolewa wakati akiwa uhamishoni, makosa ambayo alisema yalichochewa kisiasa.
Maafisa wa gereza wamesema Thaksin alisumbuliwa na shinikizo la juu la damu na asingeweza kulala usiku kutokana na maumivu katika kifua chake.
Saa chache baada ya Thaksin kurejea Thailand, mgombea wa chama Pheu Thai Srettha Thavsin alipata kura za kutosha kuwa waziri mkuu mpya, na kuhitimisha kipindi cha karibu miezi mitatu ya mivutano ya kisheria na malumbano yaliyofuatia uchaguzi wa Mei.
Srettha anatarajiwa kuidhinishwa rasmi baadae leo na mfalme wa Thailand kama waziri mkuu mpya.