Waziri mwingine Uganda apelekwa rumande kwa wizi wa mabati
17 Aprili 2023Waziri huyo ambaye alitumia mabati hayo kuezeka vibanda vyake vya mbuzi na kuku alikamatwa mwishoni mwa wiki huku mawaziri wenzake wawili wakijificha ndani ya majengo ya bunge kukwepa kukamatwa na polisi.
Picha za vibanda vya mbuzi na kuku vilivyoezekwa kwa mabati yaliyodaiwa kuwa sehemu ya shehena ya mabati ya Karamoja zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii miezi miwili iliyopita.
Soma pia: Mahakama ya Uganda yamfungulia mashtaka ya ufisadi Waziri Kitutu
Mabati hayo yalidaiwa kua mali ya seikali iliyoibwa na waziri wa nchi wa fedha na mipango ya kiuchumi Amos Lugoloobi. Hii iliibua mjadala mkubwa kuhusu kashfa hiyo, wengi wanamitandao wakimshtumu waziri huyo kwa kutumia mabati yaliyokusudiwa jamii ya wafugaji wa kuhamahama.
Siku ya Jumatatu waziri huyo alifikishwa kizimbani na kusomewa mashtaka na jaji. Waziri Lugolobi amekanusha mashtaka mawili aliyosomewa ya kupokea na kupatikana na mali ya wizi.
Museveni aahidi kuwawajibisha waliohusika na wizi
Waziri huyo alikamatwa mwishoni mwa wiki na kuzuiliwa hadi leo alipofikishwa mahakamani. Mawaziri wengine wawili wanawake waliopangiwa kukamatwa walijificha ndani ya majengo ya bunge kukwepa operesheni hiyo. Kulingana na ofisi ya kiongozi wa mashtaka, hadi sasa wameandaa mashtaka dhidi ya mawaziri 8.
Waziri wa kwanza kukamatwa wiki mbili zilizopita alikuwa Goretti Kitutu anayeshughulikia masuala ya Karamoja na siku ya Jumatano aliachiwa kwa dhamana.
Akigusia kashfa hiyo ya wizi wa mabati inahusisha mawaziri wake 22 na wabunge 31, wiki iliyopita Rais Yoweri Museveni alitaja vitendo vyao kama ufisadi wa kisiasa. Alisema kuwa atawachukulia wote waliohusika hatua za kisiasa ambazo zimefasiliwa na watu mbalimbali kuwa yamkini atawafuta kazi.
Ila hayo yataweza kuwa maamuzi mazito kwani waliohusika ni mawaziri wanaoshikilia nyadhifa nyeti ikiwemo waziri mkuu na waziri wa fedha.
Ombi la mawakili wa waziri huyo kuachiwa kwa dhamana kutokana na hali yake ya afya na umri mkubwa lilipingwa na kiongozi wa mashtaka akisema kuwa mashtaka hayo ni ya ufisadi na pana haja ya kupata muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi.
Ameongezea kuwa wanahitaji pia muda wa kutosha kuwahakiki wadhamini. Jaji amamsukuma gerezani rumande hadi tarehe 20 mwezi huu ambapo mahakama itatoa maamuzi kama aachiwe kwa dhamana.