1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Sigmar Gabriel akutana na viongozi wa Marekani

3 Februari 2017

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amekutana na mwenzake Rex Tillerson na makamu wa rais wa nchi hiyo Mike Pence mjini Washington na amebainisha kuwepo muafaka wa kisiasa baina ya nchi hizo mbili.

USA Deutschland | Sigmar Gabriel trifft Mike Pence in Washington
Picha: picture-alliance/dpaThomas Imo/Photothek.Net/Bundesregierung

Waziri Gabriel amesema ameridhika kwamba yeye na wenyeji wake ambao ni makamu wa rais Mike Pence na waziri mwenza Rex Tillerson waliweza kufikia msingi wa pamoja wa maelewano. Bwana Gabriel amesema kwamba makamu wa rais na waziri wa mambo ya nje wa Marekani wameeleza wazi kuwa wangependelea kuimarika kwa bara la Ulaya.  Baada ya kukutana na viongozi hao wawili wa Marekani, waziri huyo wa mambo ya nje ambaye pia ni naibu kansela wa Ujerumani alikutana na waandishi wa habari.

Bwana Sigmar Gabriel ndiye mjumbe wa kwanza wa serikali ya Ujerumani kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa utawala mpya wa Marekani.  Katika mikutano na wenyeji wake, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani alitetea haja ya kuendeleza biashara huru na ya haki na aliuelezea mtazamo wake wa kupinga msimamo wa rais Donald Trump wa kujenga kuta katika biashara za kuitenga Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex TillersonPicha: Reuters/C. Barria

Juu ya swala la Urusi waziri Gabriel amesisitiza kwamba vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya nchi hiyo vitaweza tu kuondolewa iwapo hatua zitapigwa katika mchakato wa kuleta amani Mashariki mwa Ukraine katika msingi wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Minsk.  

Waziri huyo wa Ujerumani amesema amekwenda Marekani sio tu kwa ajili ya kukutana na waziri mwenzake Rex Tillerson bali pia kuonyesha jinsi ushirika kati ya Ulaya na Marekani ulivyokuwa muhimu katika nyakati hizi za misukosuko. Gabriel amesema hayo pia yanahusu ushirikiano wa muda mrefu katika maswala ya usalama. 

Gabriel alisisitiza juhudi za kumaliza mapigano mabaya nchini Syria na kuendeleza majukumu katika mchakato wa amani ya mashariki ya Kati na pia kutafuta suluhisho juu ya mgogoro wa Ukraine.  Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema hakuficha chochote juu ya tofauti zilizopo baina ya Ujerumani na Marekani chini ya utawala wa Donald Trump.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/http://dw.com/p/2WtHR

Mhariri: Gakuba Daniel