Waziri Steinmeier aenda Marekani
11 Machi 2015Waziri Steinmeier alieondoka leo kwenda Marekani kwa ajili ya ziara ya siku tatu amesema Ulaya na Marekani zitakuwa na nguvu kubwa zaidi ikiwa zitasimama pamoja katika juhudi za kuitatua migogoro wakati ambapo dunia haina utulivu.Amesema msimamo wa pamoja baina ya Marekani na Ulaya utaleta manufaa kwa kila upande.
Bwana Steinmeier aliyasema hayo muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kwenda Marekani.
Waziri huyo wa Ujerumani anatarajiwa kuyajadili masuala ya Ukraine mzozo unaotokana na mpango wa nyuklia wa Iran na pia atajadiliana na wenyeji wake juu ya kitisho cha magaidi wa dola la kiislamu.
Waziri Steinmeier amesisitiza umuhimu wa kuutatua mgogoro wa Ukraine.Hata hivyo amesema umwagikaji damu umepungua kwa kiasi kikubwa.
Wamarekani wagawanyika juu ya Iran
Waziri Frank-Walter Steinmeier anafanya ziara nchini Marekani wakati ambapo mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yamefikia katika hatua nyeti. Mazungumo hayo yanatishia kuwagawanya Wamarekani.
Wakati utawala wa Obama unafanya juhudi za kufikia mapatano na Iran juu ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, Maseneta wa chama cha Republican wameandika barua kwa viongozi wa Iran na kuwatishia kwamba makubaliano yoyote ambayo Rais Obama atafikia na Iran juu ya suala la nyuklia, kabla hajamaliza muda wake mnamo mwaka 2017 yanaweza kubatilishwa.
Aliekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amewalaumu Maseneta wa chama cha Republican kwa kuiandika barua hiyo wakati mazungumzo na Iran yanaendelea. Clinton´amesema Maseneta wa chama cha Republican wanajaribu ama kumhujumu Rais Obama au wanaisaidia Iran.
Katika tamko lake leo Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameeleza kwamba katika ziara yake nchini Marekani atalijadili suala hilo na Waziri mwenzake John Kerry ,mshauri wa masuala ya usalama Susan Rice na wahusika wengine.
Mchango wa Ujerumani
Ujerumani imo miongoni mwa mataifa sita yanazofanya mazungumzo na Iran juu ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo. Ujerumani pia inatoa mchango mkubwa katika juhudi za kuutatua mgogoro wa nchini Ukraine.
Makubaliano ya mjini Minsk juu ya kusimamisha mapigano mashariki mwa Ukraine yalifikiwa pia kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Mwandishi:Mtullya abdu/rtrd,dpa,ZA
Mhariri:Yusuf Saumu