Lauterbach alenga kuhalalisha matumizi ya bangi
20 Januari 2024Hii ni licha ya upinzani ndani ya muungano wa vyama vinavyounda serikali inayoongozwa na Kansela Olaf Scholz.
Lauterbach ameliambia gazeti la Ujerumani la Die Welt kuwa, ana matumaini kuwa muswada wa kuhalalisha matumizi ya bangi utapitishwa na bunge kati ya Februari 19 na 23 na kwamba, utakuwa sheria kuanzia Aprili mosi.
Hata hivyo wabunge ndani ya chama cha Social Democrats, ambapo Lauterbach na Scholz ni wanachama, wameonyesha kutoridhishwa na hatua hiyo.
Muungano huo tawala, unaojumuisha chama cha kijani na kile cha waliberali FDP, ulikubali mwishoni mwa mwezi Novemba kuondoa bangi kwenye orodha ya vitu vilivyopigwa marufuku.
Iwapo muswada huo utapitishwa na kuwa sheria, watu wazima wataruhusiwa kupanda mimea ya bangi na kumiliki kiasi kidogo cha bangi kuanzia Aprili mosi.