1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa fedha wa Uingereza Gordon Brown ziarani Afrika.

Mohammed AbdulRahman12 Januari 2005

Kuzungumzia mpango wa kuisadia bara hilo kuondokana na umasikini

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair (kushoto) akiwa na Waziri wake wa fedha Gordon Brown
Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair (kushoto) akiwa na Waziri wake wa fedha Gordon BrownPicha: AP

Waziri wa fedha wa Uingereza Gordon Brown leo ameanza ziara ya wiki moja barani Afrika, kulipa nguvu pendekezo lake la kusaidia kulitoa bara hilo katika janga la umasikini-mpango unaofanana na ule wa"Marshall" ulioiokoa ulaya baada ya vita vya pili vya dunia. Ziara hiyo inamchukua katika nchi nne za kiafrika, kama anavyosimulia

Wote wawili-waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair na Waziri wake wa fedha Gordon Brown wamerejea mara kadhaa kuahidi kwamba wataitumia sehemu kubwa ya mwaka huu 2005, wakati Uingereza itakaposhika wadhifa wa Mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya na ule wa kundi la mataifa manane yalioendelea kiviwanda G8, kulisaidia bara la Afrika

Baada ya kusimama mjini Nairobi Kenya, Bw Brown anatarajiwa kuelekea Tanzania kesho ambako atakuweko hadi Ijumaa ambapo ataelekea Msumbiji. Hapo Jumapili atakwenda Afrika kusini, kuhudhuria kikao mjini Cape Town siku ya jumatatu cha kamisheni ya Bw Blair kuhusu Afrika yenye lengo la kushajiisha maendeleo barani humo, kabla ya kurejea nyumbani mjini London.

Wakati wa ziara yake Bw Brown atakutana na wafanyakazi wa shughuli za misaada, watu wa kawaida na mawaziri wa serikali. Waziri huyo wa fedha wa Uingereza, anatazamiwa kuitumia ziara hiyo kama zoezi la kujionea ukweli wa hali ilivyo na pia jaribio la kuupa msukumo mpango wa Uingereza kwa bara la Afrika, kwa kulipatia nafuu ya madeni, marekebisho katika sekta ya biashara na msaada.

Wakati wa ziara yake nchini Ethiopia Oktoba mwaka jana ambako alihudhuria mkutano wa Viongozi wa kamati yake kwa ajili ya Afrika , waziri mkuu wa Uingereza Blair, alitoa hotuba ya kuvutia ikifafanua juu ya juhudi za kusaidia maendeleo barani humo akiitaja hatua hiyo kuwa kipa umbele na vita vinavyopaswa kuendelezwa .

Alhamisi iliopita ,Waziri wake wa fedha Brown akafafanua mpango wake binafsi kwa bara la Afrika, akisema nchi yake itatumia wadhifa wake kama mwenyekiti wa kundi la nchi nane zilizoendelea kiviwanda, kushinikiza juu ya mpango wa kufuta kabisa madeni, nafasi za biashara na pia msaada wa fedha kwa nchi masikini sana duniani.

Bw Brown alisema nchi tajiri pia hazina budi kutatua sababu na vyanzo vya umasikini duniani kote, akipendekeza mpango unaofanana na ule uliotumiwa na waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Marekani George Marshall, kuufufua uchumi wa Ulaya ulioharibiwa wakati wa vita vya pili vya dunia.

Bw Brown amesema anaamini mwaka huu wa 2005 ni nafasi nzuri ya kuwa na mpango sawa na ule wa Marshall kwa nchi zinazoendelea. Ameutaja huo kuwa utakua ushirikiano mpya kati ya nchi tajiri na zile masikini.

Hata hivyo gazeti la Times linalotoka mjini London, limeripoti kwamba kushindwa kwa Bw Brown kupata uungaji mkono wa Marekani, kunauweka hatarini mpango wake wa kuongeza maradufu msaada wa kimataifa hadi kufikia bilioni 100, chini ya utaratibu wa msaada wa fedha wa kimataifa. Mpaka sasa mpango huo umeungwa mkono na Ufaransa na Itali lakini nchi nyengine tajiri bado hazijashawishika.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW