1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ujerumani kukutana na viongozi wa ECOWAS

5 Februari 2024

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze anajiandaa kukutana kwa mazungumzo na rais wa tume ya Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Omar Touray,mjini Abuja nchini Nigeria.

 Svenja Schulze
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze Picha: Leon Kuegeler/photothek.de/picture alliance

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze anajiandaa Jumatatu kukutana kwa mazungumzo na rais wa tume ya Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi,ECOWAS, Omar Touray,mjini Abuja nchini Nigeria.

Hayo yameelezwa na wizara yake kuhusu ziara yake katika kanda hiyo ya Afrika Magharibi. Ziara ya Schulze kwenye kanda hiyo imekuja kiasi wiki moja, baada ya kujiondowa kwa BurkinaFaso,Mali na Niger katika jumuiya ya ECOWAS wanayodai inaendeshwa kwa ushawishi wa nchi za Magharibi na kutishia uhuru wa nchi wanachama wake.

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze akizungumza na wafanyakazi wa kike wa kiwanda cha mihogo mjini AbujaPicha: Leon Kuegeler/photothek.de/IMAGO

Ziara yake inalenga kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama wa jumuiya ya ECOWAS,kuimarisha kiwango cha hali ya maisha katika eneo hilo.

Viongozi wa kijeshi pia wanasema Jumuiya ya ECOWAS, ilianzisha "vikwazo visivyo na msingi na visivyo vya kibinadamu" kufuatia mapinduzi yaliyoziondoa serikali za kiraia mamlakani.

Ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani: Baerbock aiangazia Sudan katika ziara yake ya Afrika Mashariki

Baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Niger mnamo Julai 26, ECOWAS iliiwekea vikwazo nchi hiyo na kutishia hatua za kijeshi. Nchi jirani za Burkina Faso na Mali nazo pia zinaongozwa na jeshi kufuatia mapinduzi. Nchi zote tatu zilisimamishwa uanachama ndani ya ECOWAS.

Soma pia: Ujerumani yachukua urais wa muungano wa kanda ya Sahel

Kabla ya ziara yake, Schulze alisema kuwa anajutia uamuzi wa mataifa hayo matatu, lakini akaongeza kwamba "uamuzi wake wa mataifa haya huru lazima yaheshimiwe, hata kama yatakuwa na athari kubwa za kiuchumi".