Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani ziarani Afrika kusini
9 Aprili 2010Ujumbe wa serikali kuu ya Ujerumani, unaoongozwa na waziri wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, unaendelea na ziara yake ya siku tano barani Afrika. Hii leo ujumbe huo wa serikali kuu umewasili Afrika Kusini, kituo cha pili baada ya Tanzania.
Ujerumani na Afrika kusini zinataka kuzidi kuimarisha uhusiano wao wa kisiasa na kiuchumi. Uhusiano wa kimkakati uliopo unabidi kuzidishwa, amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, baada ya mazungumzo pamoja na makamo wa rais wa Afrika, Kusini Kgalema Motlanthe, hii leo mjini Pretoria. Waziri Westerwelle amekumbusha kwamba Jamhuri ya Afrika kusini, katika Ras ya matumaini mema, ni mshirika mkubwa kabisa wa kiuchumi wa Ujerumani. Mashirika 600 ya Ujerumani yanaendesha shughuli zake nchini Afrika kusini na kuwaajiri zaidi ya watu 90 elfu.
Nchi hizi mbili kwa pamoja zinaongoza kila baada ya miaka miwili mkutano wa halmashauri ya pande mbili ambapo mada kuu zinazojadiliwa ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya kiuchumi, mazingira, utafiti na ulinzi.
Kinyume na dhamiri za awali, hakuna itifaki ya makubaliano ya serikali itakayotiwa saini wakati wa ziara hii ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, na mwenzake wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, nchini Afrika kusini. Sababu zinazotolewa ni kwamba serikali ya Afrika kusini inahitaji ufafanuzi zaidi.
Kwa mujibu wa waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, misaada ya Ujerumani kwa Afrika kusini itaongezeka na kufikia Euo milioni 112 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.Euro milioni 75 zitatumika kugharimia miradi ya nishati mbadala. Mada kuu nyengine inahusiana na mapambano dhidi ya maradhi yanayouwa kinga ya mwili-UKIMWI. Katika kipindi cha mwaka 2009, msaada jumla wa Ujerumani katika kugharimia juhudi za kupambana na ukimwi ulifikia yuro milioni 515.
Ujerumani ni mfadhili wa nne mkuu wa Afrika kusini upande huo, baada ya Marekani, Ufaransa na Uengereza.
Akihutubia halmashauri ya biashara ya nje mjini Johannesburg, waziri Guido Westerwelle amekosoa "hali ya ukosefu wa matumaini mema barani Afrika. " Waziri Guido Westerwelle amesema tunanukuu: "Katika maeneo mengi kuna dalili za maendeleo,wananchi ni vijana,wanapenda kusoma na wana motisha", amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, aliyesifu kwa kusema tunanukuu: "Mashirika ya kimataifa yanazidi kuliangalia Bara la Afrika kua ni mahala pazuri pa kuweka vitega uchumi," mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, wanapanga kukitembelea kisiwa cha Robben na kuzungumza huko pamoja na wazee wa chama cha ANC, mahakimu wa korti kuu na wanaharakati wa haki za binaadam.
Jumapili ijayo, ujumbe huo wa serikali kuu ya Ujerumani utakwenda Djibuti, kituo cha mwisho cha ziara yao ya Afrika, ambapo watazungumza na rais Ismael Omar Guelleh na waziri wa mambo ya nchi za nje, Mahmoud Ali Youssouf, kabla ya kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani wanaotumikia opereshini za kimataifa dhidi ya magaidi "uhuru wa kudumu" na zile dhidi ya maharamia wa kisomali-Atlanta-katika bahari ya Hindi.
Mwandishi: Oummilkheir Hamidou/dpa/apn
Imepitiwa na:
Miraji Othman