1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Waziri wa mambo ya nje wa Iran yuko ziarani nchini Pakistan

29 Januari 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Iran yuko Pakistan alikowasili kukutana kwa mazungumza na mwenzake Jalil Abbas kuhusu kuimaliza mivutano baada ya kutokea mashambulio yaliyofanywa na kila upande yaliyosababisha umwagaji damu.

Hossein Amirabdollahian
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein AmirabdollahianPicha: Isna

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran alitarajiwa pia kukutana na kaimu waziri mkuu Anwaarul Haq Kakar.

Mahusiano kati ya Pakistan na Iran yaliingia kwenye hatari ya kuharibika Januari 17 baada ya Iran kuanzisha mashambulizi katika eneo la mkoa wa kusini Magharibi wa Baluchistan yaliyolenga kile ambacho Iran ilisema ni maficho ya wanamgambo wanaoipinga Iran wa kundi la Jaish al Adl.

Pakistan ilisema mashambulio hayo yaliwauwa watoto wawili na wengine watatu walijeruhiwa.

Kufuatia tukio hilo, Pakistan ilimuita balozi nyumbani balozi wake wa Tehran na ikaanzisha mashambulizi ya anga katika maeneo ya ndani ya Iran katika mikoa ya Sistan na Baluchestan ambapo watu tisa waliuwawa.