Waziri wa mambo ya nje wa Libya asimamishwa kazi
28 Agosti 2023Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah amesema jana jioni katika taarifa iliyochapishwa pia kwenye mtandao wa Facebook kuwa Najla al-Mangoush "amesimamishwa kazi kwa muda" na atakuwa chini ya uchunguzi wa tume inayoongozwa na waziri wa sheria.
Wizara ya mambo ya nje ya Libya imeelezea kuwa "mkutano huo ulikuwa sio rasmi na kwamba wawili hao walipatana tu bila kupanga," japo taarifa za mkutano huo tayari zimesababisha maandamano katika miji kadhaa ya Libya.
Mzozo huo wa kisiasa ulizuka jana baada ya wizara ya mambo ya nje ya Israel kueleza kuwa, mawaziri wa mambo ya nje wa Israel na Misri walikutana wiki iliyopita.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, waziri wa mambo ya nje wa Israel Eli Cohen na Mangoush, mwenzake wa Libya, walizungumza mjini Rome katika mkutano ulioandaliwa na Waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani.
Israel imeuelezea mkutano huo kama mpango wa kwanza wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Tangu mnamo mwaka 2020, Israel imekuwa ikijaribu kurejesha uhusiano wake na mataifa kadhaa ya Kiislamu kupitia mkataba maarufu kama Abraham Accords, uliosimamiwa na Marekani.