Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Blinken aanza ziara China
17 Juni 2023Blinken atakuwa afisa wa ngazi ya juu kabisa wa Marekani kuzuru China tangu Rais Joe Biden aliingia madarakani, na waziri wa kwanza wa mambo ya nje kufanya ziara hiyo katika miaka mitano.
Blinken anawasili Beijing kesho Jumapili kwa siku mbili za mazungumzo. Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, anatarajiwa kukutana kesho na Waziri wa Mambo ya nje Qin Gang (CHIIN GANG), mwanadiplomasia mkuu Wang Yi, na pengine Rais wa China Xi Jinping siku ya Jumatatu.
Masuala mengi yatajadiliwa kuanzia kisiwa cha Taiwan, haki za binaadamu nchini China hadi Hong Kong, ubabe wa jeshi la China katika Bahari ya Kusini mwa China na vita vya Urusi nchini Ukraine. Akizungumza leo katika mkutano wake wa kampeni mjini Philadelphia, Rais wa Marekani Joe Biden amesema anatumai kukutana na Rais Xi Jinping wa China katika miezi kadhaa ijayo.